Makala

TAHARIRI: Serikali ijiandae vyema kwa sensa

January 31st, 2019 2 min read

NA MHARIRI

Huku Serikali inapojiandaa kwa shughuli muhimu ya kuhesabu watu kote nchini, kila hatua inapasa kuchukuliwa kuepusha changamoto zilizokumba zoezi kama hilo miaka kumi iliyopita. Wakati huo, matokeo kutoka wilaya nane yalibatilishwa kutokana na idadi ya watu iliyokuwa na walakini.

Shughuli ya mwaka huu ni muhimu hata zaidi chini ya mfumo wa utawala wa ugatuzi ambapo ugavi wa raslimali katika sehemu za mashinani unafanywa kwa misingi ya idadi ya watu na maeneo watokako.

Kimsingi, miradi yote ya maendeleo inaendeshwa kwa kuzingatia matokeo ya sensa. Kama ilivyo kawaida ya wanasiasa, baadhi yao wameanza kutoa vitisho kwa Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu (KNBS) wakitaka shirika hilo liendeshe shughuli hiyo kwa njia fulani.

Tunaafikiana na Waziri wa Fedha Henry Rotich anapowatahadharisha wanasiasa kupatia KNBS nafasi ya kuendesha shughuli zake bila kuingiliwa, na endapo kutakuwa na maswali, basi yawe ni kwa msingi wa ukweli na haki.

Viongozi wetu wanafahamika kutumia kila mbinu kujitanua vifua namna watu wa jamii zao walivyo wengi. Wengine hutumia mbinu chafu kuwaleta wageni kutoka mataifa jirani, bila kujali usalama wa nchi, ili waweze kuhesabiwa.

Baadhi yao wamewahi kuripotiwa kusafirisha watu kutoka eneo moja hadi jingine kwa lengo la kuzidisha idadi ya wenyeji. Habari njema ni kwamba, shirika hilo linapanga kutumia alama za vidole na maelezo mengine ambayo bila shaka yatazuia visa kama hivyo vya ulaghai.

Kuna ripoti kwamba, Wakenya wanaoishi ughaibuni huenda wakahesabiwa pia kupitia kwa ndugu na jamaa zao walioko nchini.

Hilo ni wazo zuri kwa kuwa Wakenya hao hawakomi kuwa raia wa nchi walikozaliwa kwa kuhamia nchi za ng’ambo. Lakini tungehimiza kila tahadhari ichukuliwe ili kuepusha hali ambapo jamaa hao wanatoa maelezo ya kupotosha kwa lengo la kuongeza idadi ya wanakijiji wao.

Uraia wa nchi ni swala nyeti ambalo halipaswi kuchukuliwa kimzaha. Ndiposa tunahimiza wale wanaopanga kuwasaidia wageni kuhesabiwa angalau kwa mara ya kwanza, kuweka uzalendo kwa nchi mbele.

Na kwa wale wanasiasa wanaohimiza wakazi kurejea walikozaliwa, huu ni wito potovu ambao unapalilia ubinafsi na kuzua mgawanyiko usio na maana.

Wakenya wanaoishi sehemu za miji hawakomi kuwa Wakenya hivi kwamba wanashauriwa kusafiri maeneo ya mashambani kuhesabiwa. Je, kila mkazi wa Nairobi akirejea alikozaliwa, jiji hilo litapata mgao wake wa raslimali?