Makala

TAHARIRI: Serikali ikome kuwabagua wanawake katika usajili KDF

February 14th, 2018 2 min read

Usajili wa vijana kwenye jeshi waendelea mjini Lamu Februari 12, 2018. Kati ya wanajeshi 2,000 watakaosajiliwa kote nchini, kutakuwa na wanawake kati ya 140 na 160. Wenzao wa kiume watakuwa kati ya 1,840 na 1,860. Picha/ Kalume Kazungu

Na MHARIRI

Kifupi:

  • Kati ya wanajeshi 2,000 , kutakuwa na wanawake kati ya 140 na 160. Wenzao wa kiume watakuwa kati ya 1,840 na 1,860
  • KDF yapaswa kueleza vigezo ilivyotumia kuwapatia wanawake asilimia nane pekee
  • Kuwasajili asilimia nane pekee, kutaendeleza dhana kuwa nafasi ya wanawake ni jikoni pekee

USALAMA wa nchi ni jambo ambalo halifai kufanyiwa mzaha. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiambiwa kwamba masuala ya usalama hayafai kuzungumzwa na wananchi, kwa kuwa hizo ni siri kuu ambazo maadui zetu hawafai kuzijua.

Lakini hakuna siri katika jambo hili tunalotaka kulizungumzia. Usajili wa makurutu watakaojiunga na vikosi vya jeshi letu (KDF) umefanywa kwa njia ambayo inaonekaa kukiuka mwongozo wa katiba kuhusu jinsia.

Alipokuwa akizindua usajili huo Jumatatu, Naibu Mkuu wa Majeshi Jenerali Joseph Kasaon alitangaza kwamba wanawake watakuwa kati ya asilimia saba na nane.

Kati ya wanajeshi 2,000 watakaosajiliwa kote nchini, kutakuwa na wanawake kati ya 140 na 160. Wenzao wa kiume watakuwa kati ya 1,840 na 1,860.

 

Masikitiko

Kinachohuzunisha zaidi ni kwamba KDF haikutangaza na mapema ni maeneo yapi ambako hawatarajii kusajili wanawake kujiunga na jeshi.

Kutokana na hilo, wanawake wamekuwa wakijitokeza katika viwanja mbalimbali kutaka kazi hiyo. Lakini kwa masikitiko makubwa, wamekuwa wakiambiwa kuwa hawahitajiwi.

Jambo hili linavunja mioyo Wakenya ambao wamejaaliwa kuwa na mabinti pekee. Wanaona kama walifanya makosa kuzaa watoto wa kike, ambao hawawezi kuitumikia nchi yao kwa kuilinda dhidi ya adui kutoka nje.

Jenerali Kasaon ana wajibu wa kuwaeleza Wakenya kuanzia leo, ni maeneo gani yaliyosalia ambako wanawake hawatasajiliwa. Kauli hiyo ikitangazwa hadharani, itasaidia watu kuokoa muda, nauli na nguvu zao kurauka asubuhi na mapema na kwenda katika viwanja vya usajili.

 

Thuluthi mbili

Pia tunajua kwamba kwa vile Katiba inasisitiza kusiwe na zaidi ya thuluthi mbili za jinsia moja, KDF yapaswa kueleza vigezo ilivyotumia kuwapatia wanawake asilimia nane pekee.

Jambo hili lafaa kuangaliwa kwa makini na haraka. Ikiwezekana, Mkuu wa Majeshi Jenerali Samson Mwathethe anapaswa kuingilia kati, ili idadi ya wawake katika jeshi letu angalau ifikie asilimia 15.

Tunajua kuna wanaoamini kuwa wanawake wengi wana mioyo ya huruma na hawawezi kwenda vitani. Lakini kuwasajili asilimia nane pekee, kutaendeleza dhana kuwa nafasi ya wanawake ni jikoni pekee.

Dhana hii ikiendelezwa, itarejesha nyuma hatua tulizopiga katika kuhamasisha wanawake kufanya kazi za jinsia ya kiume.