Makala

TAHARIRI: Serikali ingezingatia hali ya shule kabla ya masomo kurejelewa

October 9th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

TANGAZO la Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, Jumanne kwamba shule zitafunguliwa upya Jumatatu ijayo, liliwapata wazazi wengi ghafla.

Ni tangazo ambalo pia limezua hofu miongoni mwa wadau kadha wa elimu, baadhi wakilalama kwamba hawakushirikishwa kikamilifu kabla ya uamuzi huo kufikiwa.

Ingawa ni wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne pekee wanaorejelea masomo yao, wizara ingezingatia hali ilivyo katika baadhi ya shule.

Kwa mfano, katika eneo la Nyanza, hasa Kaunti ya Kisumu, baadhi ya shule zimeathiriwa na mafuriko, kiasi kwamba hakuna anayeweza kufika zilipo.

Katika eneo la Bonde la Ufa, kiwango cha maji kimeripotiwa kuongezeka katika baadhi ya maziwa kama vile Ziwa Nakuru, Ziwa Naivasha na Ziwa Baringo, hali ambayo imeziathiri baadhi ya shule zilizo maeneo yaliyo karibu nayo.

Kaskazini Mashariki, kumekuwa na changamoto kuhusu usalama miongoni mwa walimu na wanafunzi, hali inayochangiwa pakubwa na mashambulio yanayotekelezwa mara kwa mara na makundi ya kigaidi.

Tatizo kama hilo limekuwa likishuhudiwa katika eneo la Pwani.

Bila shaka, haya ni masuala yenye uzito, ambayo serikali ilifaa kuyaangazia kabla ya kutoa tarehe ya ufunguzi rasmi wa shule.

Ingawa ni matatizo yaliyokuwepo hata kabla ya janga la virusi vya corona kuzuka nchini, ingekuwa vyema ikiwa serikali ingebuni utaratibu mpya kuyakabili.

Katika baadhi ya shule, imeibuka huenda hata tatizo la kuwalisha wanafunzi likaibuka kutokana na athari za kiuchumi za corona.

Je, mbona serikali imeyanyamazia masuala kama haya? Imani yetu ni kwamba, ingekuwa bora serikali kujumuisha masuala hayo kuwa miongoni mwa mambo itakayoyapa kipao mbele wanafunzi watakaporejea shuleni.

Tunapozingatia utekelezaji wa masharti ya kudhibiti maambukizi ya corona, ni muhimu pia mahitaji ya kimsingi ya wanafunzi yazingatiwe, kwani yatakuwa na athari kubwa kuhusu ikiwa hatua hiyo itafaulu au la.

Hilo ndilo litahakikisha ufunguzi wa shule utakuwa shwari, bila kukumbwa na changamoto zozote. Muhimu ni kuhakikisha hakuna yeyote atahisi kudhulumiwa. Kunafaa kuwa na usawa.