Makala

TAHARIRI: Serikali isaidie polisi kuepuka maafa tele

October 14th, 2019 1 min read

Na MHARIRI

VISA vya polisi kushambuliwa kwa mabomu yaliyotegwa barabarani vinazidi kuongezeka.

Hali hii inastahili kuchukuliwa kwa uzito na asasi zote husika serikalini kwani polisi wanafaa kufanya kazi kwa njia itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao ya kulinda raia.

Kupokea habari kwamba polisi 11 wamefariki katika shambulio aina hii ni jambo linalosikitisha sana.

Hivi majuzi, tulipoteza polisi wengine saba katika njia hiyo hiyo, kukawa na ghadhabu sawa na jinsi ilivyo sasa kutoka kwa raia lakini hatuoni hatua zozote mwafaka zikiwekwa na serikali kukomesha au hata kupunguza matukio haya.

Maeneo yanayolengwa zaidi na mabomu hayo yanayoaminika kutegwa na wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab, ni yale yaliyo kwenye mpaka wa Kenya na Somalia maeneo ya Lamu, Garissa na Mandera.

Hali hii si salama pia kwa raia wanaotumia barabara hizo, ikikumbukwa kwamba kuna wakati dereva wa gari la kampuni ya Kenya Power aliponea chupuchupu bomu aina hiyo lilipomlipukia barabarani.

Haya yote hutokea ilhali idara ya polisi ilinunua magari yanayoweza kustahimili milipuko ya bomu miaka michache iliyopita.

Kila wakati maswali yanapoibuka kuhusu mahali magari hayo yanatumiwa, au kama yalikuwa duni, idara ya polisi hujitetea kwamba yalikuwa machache na yanatumiwa katika maeneo mengine ya nchi.

Haieleweki kwa nini serikali inaona wazi hatari inayokodolea maafisa wetu wa polisi wanaposhika doria katika maeneo ya mipaka na bado wanaachwa kutumia magari ya kawaida na kuangamia bomu linapolipuka barabarani.

Zaidi ya haya, inafaa wakuu wa polisi wafanye utathmini upya kuhusu hali ya ukusanyaji habari za kijasusi katika maeneo hayo.

Ingawa tunafahamu kuna visa vingi vya kigaidi vilivyozuiliwa kufuatia ukusanyaji bora wa habari za kijasusi, bado kuna pengo linalohitaji kuzibwa.

Magaidi wanapoweka mitego ya mabomu barabarani kusubiri gari la polisi kupita, inamaanisha wanajua mengi kuhusu upigaji doria wa polisi hao.

Ni kupitia kwa mbinu bora za ujasusi ambapo itabainishwa kama kuna watu wanaopasha magaidi habari kuhusu shughuli za polisi.