Makala

TAHARIRI: Serikali ishughulikie ripoti ya uchafuzi

August 15th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

RIPOTI ya uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo kuhusu uharibifu wa mazingira yafaa kuchunguzwa kwa makini na wadau, ili suluhu ya haraka ipatikane.

Uchunguzi huo uliodhaminiwa na kampuni ya Nation Media Group na kuwahusisha wanasayansi wa mazingira, unaonyesha kuwa huenda mamilioni ya Wakenya wakawa katika hatari ya kuambukizwa maradhi kama kansa.

Ilibainika kuwa maji ya Mto Nairobi ambao baadaye kushikana na Mto Athi na mwishowe Sabaki kabla ya kuingia Bahari Hindi, yana kemikali hatari zinazoweza kusababisha madhara makubwa kwa miili ya binadamu.

Kwa mfano iligunduliwa kuwa maji hayo yana kemikali za viwandani, uchafu kutoka kwa vyoo, vijusi vilivyotupwa kati ya vitu vingine hatari. Lakini ni maji hay ohayo yanayotegemewa na wakulima kunyunyiza mashamba yao wanapokuza Sukuma wiki, makabeji na mimea mingine inayotumiwa na binadamu.

Katika maeneo ya Ukambani, maji hayo hutumiwa na wakazi wa Machakos na Makueni kunywesha mifugo yao. Hata watu huogelea au kuyatumia kwa matumizi mengine ya nyumbani.

Wataalamu waligundua viwango vya juu mno vya kemikali kwenye kaa na Wanyama wengine wa baharini eneo la Sabaki katika Kaunti ya Kilifi. Kemikali hizo, mtu anapozimeza zinaweza kusababisha kansa au maradhi mengine yanayouathiri mwili kwa asilimia kubwa.

Kutolewa kwa ripoti hii kwafaa kuwafungua macho wakuu serikalini, hasa maafisa wa Shirika la Kulinda Mazingira (NEMA). Maafisa hao hawajaonekana kutekeleza wajibu wao ipasavyo. Wanaonekana kuidhinisha viwanda kujengwa na hatimaye kutoa ripoti ya usalama wa mazingira bila ya kuwa na ushahidi wa maeneo ambako viwanda hivyo vitatupa uchafu.

Si ajabu kuwa kansa imesambaa Kenya na inaendelea kuua wananchi bila ya kupatikana suluhu. Wakati wa ibada ya wafu ya aliyekuwa Gavana wa Bomet, Dkt Joyce Laboso, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa serikali itaanzisha vituo vya kutibu saratani.

Vituo hivyo havitakuwa na maana kwa Wakenya ikiwa serikali haitaanza na kuwakabili watu wanaochafua mazingira, hasa mito mikuu humu nchini.

Wakati wa marehemu John Michuki, wananchi waliona juhudi za serikali kukabiliana na uchafuzi huo. Ni kwa nini sasa hivi jambo hilo haliwezekani?