Makala

TAHARIRI: Serikali isisahau mazao mengine

July 3rd, 2020 2 min read

Na MHARIRI

NCHI nyingi zilizopiga hatua kimaendeleo, zimefanya hivyo kutokana na kuthamini kilimo.

Ni kupitia kilimo ambapo bidhaa kama pamba zilitumika kuanzisha ustawi wa viwanda Ulaya.

Ni kupitia bidhaa za kilimo ambapo viwanda vinaweza kuendelezwa, kwa kuwa hata baada ya kufanya kazi kwa bidii, wafanyakazi watahitaji chakula na vinywaji. Chai, kahawa, uji, na bidhaa nyingine, zinatokana na kilimo.

Hapa Kenya, tumekuwa tukiimba kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa nchi, bila kuonyesha kauli hiyo kwa vitendo.

Kilimo cha mahindi, majanichai, kahawa, parachichi, maembe, korosho, nazi, miwa na kadhalika, kimechukuliwa kuwa jambo la kawaida tu.

Wakulima wa mahindi kwa mfano, wamekuwa wakihangaika kupata mbolea ya bei nafuu. Wanapoipata, huvamiwa na viwavi na wadudu wengine wanaoharibu mimea. Wakifanikiwa kuvuna, hukosa bei kutokana na kuingizwa kwa mahindi kutoka nchi za nje. Hali ni sawa na hiyo kwa wakulima wa miwa na wafugaji wa kuku wa mayai na wenzao wa ng’ombe wa maziwa.

Kwa hivyo hatua ya Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya kupiga marufuku uagizaji sukari kutoka nje kama sehemu ya hatua za kuokoa sekta ya sukari nchini, ni wa kupongezwa.

Serikali kupitia hatua hiyo, ilifuta leseni zote za uagizaji sukari ambazo hutumiwa na wafanyabiashara kuingiza sukari nyingi nchini kupita kiasi. Sukari inayoagizwa kwa ajili ya matumizi nyumbani haitaruhusiwa nchini.

Wakulima wa miwa katika eneo la Magharibi mwa nchi wameendelea kuzama kwenye umasikini huku viwanda vya miwa vikisimamisha shughuli. Kampuni za sukari zimedinda kununua miwa ya wakulima hao kwa sababu zina sukari nyingi ambayo hazijauza.

Kuingizwa kwa sukari nchini, kimagendo, kutoka Uganda na Somalia kunaathiri sekta ya sukari nchini.

Kutelekezwa kwa wakulima wetu kupitia kuruhusu wafanyibiashara wachache kuuza bidhaa za bei ya chini, kumesababisha wakulima wa majani chai na kahawa kukata mimea yao na kuingilia kilimo mbadala.

Wakulima wa maeneo mengine, kama Pwani ambao hukuza minazi, korosho, maembe, machungwa na mazao mengine yanayoweza kuuzwa kimataifa vilevile wameendelea kupuuzwa.

Inaposhughulikia sukari, serikali haifai kusahau wakulima wengine, wanaopitia masaibu zaidi ya hayo.