Makala

TAHARIRI: Serikali isiwaadhibu wazazi

February 19th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

SHUGHULI inayoendelezwa na serikalli ya kuwasaka wanafunzi wajiunge na shule za upili ni muhimu kwa nchi.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi kuwa hakuna mwanafunzi atakayepita mtihani katika darasa la nane na akose kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Kulingana na Waziri wa Elimu, Bi Amina Mohamed, wanafunzi wote waliofanya mtihani huo mwaka jana walipaswa kujiunga na shule, ili waendeleze masomo.

Wazazi ambao wameshindwa kupeleka watoto hao shuleni wamejikuta wakisakwa kwa usaidizi wa machifu. Kupitia msako huo, baadhi ya wazazi wameshtakiwa mahakamani kwamba wamekataa kuwapeleka watoto wao shuleni. Sababu ambazo serikali inatoa ni kuwa shule za upili za kutwa hazilipishwi chochote cha ziada.

Kauli hiyo ya serikali si ya kweli. Ingawa shule za upili za kutwa hazina gharama kubwa, bado kuna wazazi ambao hawana uwezo wa kifedha wa kuwawezesha kununua baadhi ya mahitaj yanayohitajika.

Ingawa wazazi hawaitishwi karo, kuna mambo muhimu kama sare za wanafunzi, vitabu na malipo mengine ambayo hata serikali huwa haina habari kuyahusu.

Kwa mfano hata sasa kuna walimu wa shule za upili ambao huwaagiza wazazi wanunue sare kutoa maduka fulani. Maduka hayo mara nyingi huwa yanauza sare hizo kwa pesa nyingi kuliko katika maduka mengine.

Serikali inasema imepeleka vitabu katika shule lakini hilo halijawazuia walimu wakuu kuitisha kamusi za Kiingereza na Kiswahili, ambazo bei yake si chini ya Sh1,000 kila moja.

Wazazi huitishwa reki, upanga, mti wa kuchezea hoki au hata mpira. Shule zilizo na mabasi huitisha pesa za kulipia bima au ya basi ikidaiwa kuwa lilinunuliwa kwa mkopo.

Kwa mizingi hiyo, si rahisi kwa mzazi ambaye anatoka katika eneo lenye umasikini kumudu gharama ya kumpeleka mwanawe katika kidato cha kwanza.

Ni makosa na kukosa kuelewa mambo kwa serikali kuwakamata wazazi kwa kisingizio kuwa wanakataa kupeleka watoto shuleni.

Maafisa wa serikali wanapaswa kuwatumia maafisa wa kurekebisha tabia, kuchunguza na kuelewa maisha ya wazi hao kabla ya kuwachukulia hatua.

Hakuna mzazi anayesomesha mwanawe hadi darasa la nane halafu akatae kumpeleka katika shule ya upili.

Serikali yapaswa kuwatuma maafisa wa Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) na wenzao wa Upelekezi (DCI), wachunguze ni kwa nini wabunge na viongozi wengine waliopewa pesa za basari, hawajazitumia kusaidia watoto katika maeneo yao kupata elimu.