Makala

TAHARIRI: Serikali isiwatie hofu watahiniwa

November 12th, 2018 1 min read

NA MHARIRI

MTIHANI wa Kidato cha Nne (KCSE) unapoingia wiki ya pili, kuna mengi ambayo tumejifunza.

Kinyume na miaka ya nyuma, wakati huu juhudi zimeimarishwa kufanya mtihani huo uwe wa kuthaminiwa. Miongoni mwa juhudi hizo ni kuweka maafisa wa usalama kwenye maeneo karatasi za mtihani zinapohifadhiwa shuleni.

Lakini hata baada ya mbinu hizi mpya, zipo taarifa za kunaswa walimu, maafisa wa usalama na hata wazazi wakijaribu kudanganya wakati mtihani unapoendelea.

Ni juzi tu ambapo mwanafunzi katika shule moja ya upili eneo la Pangani, Nairobi, alikamatwa akiwa na simu ndani ya chumba cha mtihani.

Hii inaonyesha kuwa maafisa wanaosimamia mtihani si waangalifu. Ama kama wako makini, basi kuna ukora unaoendelezwa katika baadhi ya vituo vya mithani hiyo.

Ukora huu wa watu wachache haufai kutumiwa kuwahangaisha watahiniwa wengi waaminifu.

Kinachokera zaidi ni kitendo cha serikali kuwaathiri kisaikolojia wanafunzi wasiohusika na udanganyifu huo kwa kuwavamia kwa njia inayowatia uoga.

Mawaziri, makatibu na maafisa wasimamizi was taasisi zinazohusika na elimu na mitihani wanaendeleza vitisho hivyo.

Je, mwanafunzi wa shule ya msituni kabisa ambako gari la serikali linapoonekana huwa labda kuna mshukiwa wa uhalifu anasakwa, atahisi vipi akivamiwa na Waziri wa Usalama?

Madai ya wakuu wa Chama cha Walimu wa Upili (KUPPET) kwamba ziara za wakuu serikalini zinawaathiri watahiniwa, hazifai kupuuzwa.

Imebainika kuwa baadhi ya maafisa hao huvuruga muda wa mtihani kwa kupiga picha za selfi na watahiniwa. Hata kuna siku Naibu Rais William Ruto aligawa karatasi za KCPE kwa watahiniwa wa shule moja ya msingi.

Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) lapaswa kuangalia upya sera zake kuhusu wanaofaa kuingia ndani ya vyumba vya mitihani.

Ilivyo kwa sasa, tunatumia mbinu za kijeshi dhidi ya maelfu ya watoto wasiofahamu chochote kuhusu udanganyifu kwenye mitihani.

Tiba kwa wizi si kuwatishia watahiniwa, ila kuweka sera na mikakati madhubuti itakayoziba mianya yote ya udanganyifu.