Makala

TAHARIRI: Serikali isiyaruhusu magenge ya uhalifu

February 19th, 2018 2 min read

Msimamizi wa mpango wa Nyumba Kumi Bw Joseph Kaguthi. Picha/ Maktaba

Na MHARIRI

SERIKALI yapaswa kuwaondolea wasiwasi wananchi kuhusiana na habari za kuibuka magenge yanayoshiriki katika mpango wa kuwalinda watu, maarufu kama ‘Nyumba Kumi’.

Mpango huo ulioanzishwa baada ya kuzuka ongezeko la mashambulizi ya kigaidi, ulilenga kuwezesha wananchi kuwajua majirani zao walio nyumba kumi kutoka kwa nyumba zao.

Ilitarajiwa kuwa kupitia mpango kama huo, wakazi wangewajua majirani zao kwa majina, na kuchunguza mienendo isiyokuwa ya kawaida ili kuwafahamisha maafisa wa usalama.

Iligundulika kuwa, wengi kati ya waliohusika na vitendo vya kigaidi walitajwa kuwa watu wapole, ambao hawangeweza hata kumuua nzi. Lakini baadhi pia ni wageni waliokuwa wakiwatembelea wakazi na kukaa kwa muda.

Kwa hivyo alipopewa jukumu la kusimamia mpamgo huo, Bw Joseph Kaguthi alitarajiwa kutumia ujuzi wake wa miaka mingi katika utawala, kuangamiza kabisa vikundi vya uhalifu katika makazi.

 

Kero

Hata hivyo, imebainika kuwa badala ya mpango huo wa ‘Nyumba Kumi’ kuwahakikishia wananchi usalama wao, sasa umegeuka kuwa kero baada ya kuingiliwa na makundi ya wahalifu.

Takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 2017  pekee zaidi ya watu 600 waliuawa na magenge hayo. Inadaiwa kuwa, magenge hayo ambayo wanachama wengi ni vijana wasiokuwa na ajira, yamegauka kuwa viongozi wa mashtaka na majaji wakati mmoja.

Katika maeneo kama Kirinyaga na Kisii, vijana walio kwenye mpango wa ‘Nyumba Kumi’ huwashambulia washukiwa kwa marungu, mateke n ahata silaha butu na kuwapiga hadi kuwaua.

Kwa kufanya hivyo, watu hao wanakuwa wahalifu hata kuwashinda wahalifu wanaopaswa kuwazuia.

Kwa sababu hii, ipo haja kwa serikali kutathmini upya uanachama wa wanaokaa kwenye kamati za ‘Nyumba Kumi’.

 

Kamati zivunjwe

Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i anapaswa kuvunja mara moja kamati zote nchini, na kupiga msasa kwa kuchunguza mienendo ya uhalifu ya watu kabla ya kujiunga na mpango huo wa usalama.

Polisi pia wana wajibu wa kuwatia nguvuni watu wanaowavamia wakazi na kuwaua kwa kisingizio cha kukabiliana na uhalifu. Sheria za nchi hii ziko wazi kuhusu wajibu wa wanaosimamia usalama.

Hakuna mtu yeyote kwenye mamlaka ya kuwaua wenzao, hata kama kutakuwa na ushahidi kuwa wanahusika na uhalifu.