Makala

TAHARIRI: Serikali italazimika kulinda wanafunzi

October 7th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

BAADA ya kuahirisha ufunguzi wa shule na taasisi nyinginezo za elimu mara kadhaa, hatimaye Serikali imeamua kuzifungua juma lijalo japo kwa awamu.

Jumanne, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alitangaza kufunguliwa kwa kidato cha nne, darasa la nane na daraja la nne kuanzia Jumatatu tarehe 12 Oktoba.

Tangazo hilo, japo limewapata wazazi na wanafunzi wengi wakiwa hawajajiandaa vizuri, linawalazimu waanze kujitayarisha kuwarejesha watoto wao shuleni; lisilobudi hubidi eti.

Sharti tukiri kwamba hali shuleni haitakuwa shwari wala kawaida, hivyo basi kuwahitaji walimu, wanafunzi, wazazi na wadau kwa pamoja kuwa waangalifu zaidi ili kuzuia kusambaa kwa ndwele ya Covid-19 ambayo husababishwa na virusi hatari vya corona.

Yapo mambo kadhaa yanayofaa kubainishwa wazi na serikali kabla ya watoto kufungua shule.

Suala la kwanza, kutokana na juhudi za kuzuia corona, bila shaka gharama ya elimu itaongezeka.

Patachipuka gharama za maski, sanitaiza na nyinginezo katika jitihada za kuhakikisha wanafunzi hawaambukizani ugonjwa huo hatari uliosababisha mkwamo wa shughuli nyingi nchini na duniani kote.

Maadamu wapo wazazi wengi tu waliokuwa wakitatizika kimapato hata kabla ya corona, na wengine wengi ambao wameathirika kiuchumi kutokana na janga hili, itakuwa vyema iwapo serikali itasimamia baadhi ya gharama ili kuwezesha wanafunzi wengi iwezekanavyo kuendelea na masomo yao.

Ni muhimu serikali ieleze bayana imejiandaa vipi kusimamia gharama hizo za ziada hasa ikizingatiwa kuwa imewashtukiza wazazi kwa kufungua shule ghafla mwezi huu Oktoba.

Ikumbukwe wazazi wengi walipoambiwa na serikali kuwa shule zitafunguliwa Januari, waliondoa gharama za elimu katika mipango yao.

Kwa kuwarejesha ghafla, wazazi wengi watatatizika kupata karo, achilia mbali gharama za ziada kama vile maski na vieuzi.

Ushauri wa Prof Magoha kwamba watakaoshindwa kulipa karo wahamishie watoto wao katika shule za umma hauna mashiko maadamu tayari idadi ya watoto katika shule hizo ni kubwa zaidi tayari.

Mambo mengine muhimu ni kutangaza kanuni zitakazofuatwa na wanafunzi wawapo shuleni, mipango ya dharura ya kuwasaidia watoto watakaoambukizwa na mikakati ya jumla ya kuepusha mkurupuko wa pili wa ugonjwa huo.