TAHARIRI: Serikali iunde sera wakongwe wafunze vijana wakiwa kazini

TAHARIRI: Serikali iunde sera wakongwe wafunze vijana wakiwa kazini

NA KITENGO CHA UHARIRI

MSWADA wa wakongwe Spesheli ulio bungeni, una umuhimu mkubwa kwa wakongwe, katika nchi ambayo punde watu wanapostaafu, hutengwa na jamii na kuwa na wakati mgumu kujikimu.

Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kiambu Gathoni wa Muchomba kwenye mswada huo, alipendekeza kuwa serikali iwape wakongwe waliotimu miaka 60, huduma za matibabu bila malipo katika hospitali za kitaifa na zile za kaunti.

Lakini pia kuna kipengee kinachopendekeza kwamba wakongwe waliokuwa wakifanya kazi serikalini wakastaafu wakiwa na ujuzi katika sekta muhimu, warejeshwe kazini.

Kama mtu alikuwa daktari, polisi, mwanajeshi au Mwalimu na kumetokea dharura, ni kawaida kote ulimwenguni kwamba anaweza kurejea kwa muda.

Nchini Marekani, Uingereza na kwingine, watu kama hao huitwa kujitolea na kusaidia nchi kukabili janga fulani. Kwa mfano kunapozuka vita au mlipuko wa maradhi kama vile corona, huwa wanaitwa kazini, lakini kama watu wa kujitolea.

Hapa Kenya, kuwapa wakongwe wastaafu fursa ya kufanya kazi tena kuna manufaa yake. Kwanza wakati huu ambapo mpango wa kuwapa Sh2,000 kwa mwezi umekuwa ukiwacheleweshea pesa kwa hata miezi mitano, pesa watakazopata zitawasaidia kujitegemea. Pili, wana tajriba ya kutosha katika masuala wanayoshughulikia. Lakini inaishia hapo.

Kama ni shuleni, sasa hivi kuna mfumo wa CBC ambao wengi au baadhi yao hawajafunzwa jinsi ya kuuendeleza. Kwa madaktari, teknolojia imepanuka. Kuna tiba inayofanywa kutpitia Zoom au mawasiliano ya video Telemedicine. Pia kuna Apu nyingi za matibabu kama vile M-Dawa na kadhalika. Haya si mambo ya kuyaelewa kwa makini kwa siku chache.

Kinachohitajika serikalini ni kuunda sera maalumu kuhusu ukuzaji vipawa kazini. Kama wakongwe hao walikuwa na ujuzi siku hizo, je, hawakuwa na watu chini yao? Serikali ilifanya nini kuhakikisha kuwa waliwafunza wenzao kabla ya kustaafu?

Isitoshe, kuna maelfu ya vijana waliofuzu vyuoni ambao huambiwa hakuna ajira. Kama kweli wabunge wanataka kuhakikisha kunapatikana watu wenye ujuzi kila mara, basi waweke sera kuhusu utoaji mafunzo kazini.

Vijana wengi wanapoajiriwa, mara nyingi huwa wanatelekezwa na wazee, ambao huwachukulia kuwa tisho kwa ajira zao. Badala ya kuwachukulia kuwa wafanyikazi wenza, huwaangalia kama maadui.

Viongozi wanaoahidi vijana ajira kwenye mikutano yao ya kampeni, wanapaswa kuanzia hapa.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Wanaomezea ugavana wajue kazi yahitaji...

GWIJI WA WIKI: ALVINS KASUKU

T L