Makala

TAHARIRI: Serikali iunge juhudi za kuwalinda watoto

May 21st, 2020 2 min read

Na MHARIRI

WAKATI huu ambapo zaidi ya watu 1,000 wameambukizwa virusi vya corona nchini, mojawapo ya njia za kukabili maambukizi ni kuvaa barakoa.

Takwimu zilizotolewa na Waziri Mutahi Kagwe siku ya Jumanne, zilionyesha kuwa kati ya watu walioambukizwa corona, kuna idadi kubwa ya watoto walio na umri wa chini ya miaka kumi.

Kwa bahati mbaya, kwenye mpango wa serikali wa kutengeza barakoa, hakujakuwa na mikakati ya kuwezesha au kuagiza viwanda kutengeza vifaa vya kutumiwa na watoto.

Watoto wengi katika miji humu nchini, hurandaranda bila barakoa kwa sababu wanaozitengeza huzingatia tu za kuvaliwa na watu wazima.

Kwa hivyo, kujitokeza kwa mama ambaye anaunda barakoa hizo kwa watoto ni hatua nzuri.

Mama huyo, Bi Linah Oketch, inasemekana ameanza kuunda barakoa za kutumiwa na watoto katika Kaunti ya Mombasa.

Kaunti hiyo mbali na kuongoza kwa idadi ya vifo, Jumatano ilikuwa na visa 30 vipya vya maambukizi kati ya watu 66 waliotangazwa kuwa na Covid-19 kote nchini.

Bi Oketch anasema alichukua hatua hiyo baada ya kuwaona wazazi wakiwa wamevaa barakoa, wakitembea na watoto wao ambao hawajikingi.

Tunapohimiza mafundi cherehani wengine waige juhudi zake, serikali kupitia wizara za Afya na ile inayohusika na uvumbuzi, yapaswa kuwawezesha wawekezaji wadogo wanaofanya mambo yenye manufaa kwa nchi.

Wabunge wa kike katika kaunti zote 47 hupokea pesa za kuwawezesha akinamama wenzao. Wale wanawake wanaojitolea kuendeleza juhudi za serikali kupambana na maambukizi, wanahitaji kuungwa mkono kifedha.

Aidha, wizara ya Afya yapaswa kuwa macho na kuwatuma maafisa wake katika vituo vya magari ya usafiri wa umma, hasa mijini. Imeibuka kuwa, baadhi ya wahudumu wa matatu hushirikiana na wahuni na kuwaibia wateja.

Kuna ripoti kuwa katika jiji la Nairobi, baadhi ya wahuni wamekuwa wakiwanyunyizia watu ‘sanitaiza’ ambayo huwalaza na hatimaye kuwaibia.

Wiki hii Mamlaka ya Ubora wa Bidhaa (KEBS), ilipiga marufuku aina nane za sanitaiza kwa kuwa havijafikia viwango vya ubora unaohitajika.

Kupiga marufuku pekee hakutoshi. Sanitaiza hizo yafaa zikusanywe na kuharibiwa, kabla hazijapenya kijanja na kuwaathiri watu.