TAHARIRI: Serikali iwaombe radhi wanariadha

TAHARIRI: Serikali iwaombe radhi wanariadha

KITENGO CHA UHARIRI

KENYA ni miongoni mwa nchi zilizofanya vyema duniani kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyokamilika Jumapili iliyopita jijini Tokyo, Japan.

Wazalendo na ma shujaa wa Kenya walishinda mataji manne ya dhahabu, fedha pia manne na shaba mbili katika mashindano hayo ya hadhi zaidi ulimwenguni kwenye riadha.

Kenya ilizoa dhahabu kupitia kwa Eliud Kipchoge na Peres Jepchirchir (marathon), Emmanuel Korir (800m) na Faith Chepng’etich (1500m).

Brigid Kosgei (marathon), Hellen Obiri (5000m), Ferguson Rotich (800m) na Timothy Cheruiyot (1500m) walizoa nishani za fedha nao Benjamin Kigen na Hyvin Kiyeng wakaridhika na shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Licha ya ufanisi huu uliofanya Kenya kumaliza kileleni Barani Afrika na nafasi ya 19 ulimwenguni, wanariadha wetu waliwasili nchini kimya kimya bila mapokezi mazuri yaliyowafaa kulingana na jinsi walivyong’aa Tokyo.

Alipotua katika uwanja wa ndege wa JKIA saa tisa asubuhi ya kuamkia Jumatano, Bw Kipchoge ambaye ni mwanariadha wa tatu ulimwenguni kutetea rekodi yake ya olimpiki katika mbio za marathon, alipokolewa tu na wanahabari wachache wala hakukuwa na hata afisa mmoja wa ngazi ya juu serikalini kumlaki.

Ni wanahabari hao wachache ambao walimhoji kuhusu iwapo analenga kustaafu kabla ya kushiriki Olimpiki ijayo.

Hata Bw Kipchoge alionekana kushangazwa na mapokezi hayo na huenda hilo lilikuwa kiini cha majibu makali aliyowapa wanahabari hao.

Iweje wanariadha kutoka nchi jirani ya Uganda ambao walishinda medali mbili pekee ya dhahabu na nyingine mbili za shaba pekee wapewe mapokezi ya heshima ilhali hapa wanariadha wetu hawathaminiwi licha ya kufanikiwa kwao?

Nchini Uganda, Rais Yoweri Museveni aliwalaki wanariadha hao na hata kuwaalika ikuluni ambako inatarajiwa watatuzwa vyema kuwa kuipa nchi hiyo sifa.

Hali ni kinyume hapa nchini na yaonekana kama taifa tumezoea ushindi kwenye riadha kiasi kwamba wanariadha wetu sasa hawathaminiwi tena.

Wizara ya Michezo inafaa kuwaomba Wakenya radhi kuhusu tukio hili na ipange ratiba na ikulu ili wanariadha wetu watambuliwe na watuzwe na Rais Uhuru Kenyatta kwenye hafla ambayo itapeperushwa na runinga zote hapa nchini.

You can share this post!

KNUN yadai wazo la kuruhusu matatu kubeba asilimia 100 ya...

DIMBA MASHINANI: Parklands Simba yajivunia mafanikio...