Makala

TAHARIRI: Serikali iwasikize wanaoandamana

August 25th, 2020 1 min read

Na MHARIRI

TANGU kituo cha runinga cha NTV kifichue kuwepo ufujaji wa pesa za kusaidia kukabiliana na janga la Covid-19, Wakenya wameendelea kujitokeza kukemea wizi huo.

Makundi ya wahudumu wa afya, wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na wadau wengine, yametoa kauli kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Miongoni mwa mbinu zinazotumiwa kuwasilisha ujumbe huo ni kuandamana barabarani, na kuwasilisha malalamishi kwa wakuu na idara zilizo na mamlaka ya kuchukua hatua zinazotakiwa.

Kwa mara ya pili jana, polisi walitumiwa kutawanya waandamanaji na kuwakamata baadhi yao. Hatua hiyo inasemekana kuchukuliwa kwa kuwa waandamanaji walikiuka kanuni za kudhibiti maambukikzi ya Covid-19.

Maafisa wanne waliokuwa wakiongoza maandamano mjini Nakuru walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kati.

Kukamatwa kwa wanaharakati hao na Wakenya wengine wanaoendelea kupaza sauti zao dhidi ya maovu, kunaonekana kunafanywa kwa nia fiche.

Sababu kuu ya Wizara ya Afya kukataza watu kukusanyika kwa wingi, ni kuchunga kwamba kusiwe na uwezekano wa baadhi yao kuambukizwa kwa kutovaa barakoa.

Tangu wiki jana, waandamanaji wamekuwa wakieleza ujumbe wao kupitia mabango. Isitoshe, wamekuwa wakitembea wakiwa wameacha hatua kutoka mmoja hadi mwengine. Katika hali kama hiyo, hakuna uwezekano wa watu hao kuambukizana.

Kwa siku kadhaa sasa, takwimu za maambukizi ya Covid-19 zinaonyesha kupungua kwa virusi hivyo.

Jumatatu kwa mfano, kulikuwa na watu 193 pekee walioambukizwa, ikilinganishwa na wakati ambako kwa siku idadi ilikuwa haipungui watu 700.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa viwango vya maambukizi vimepungua na kwa hivyo, maadamu watu wanazingatia kanuni muhimu, wana haki ya kusikizwa.

Isitoshe, kukusanyika kwa wanaharakati hao hakuna tofauti na mpango wa serikali kuwakusanya wanafunzi mwezi ujao, ili wasome kwenye kumbi za kijamii.

Kinachofaa kuzingatiwa katika maandamano haya, ni ujumbe unaopitishwa na wananchi; kwamba wamechoshwa na ongezeko la visa vya ufisadi. Ujumbe huo wastahili kupokewa na kushughulikiwa kwa makini na idara husika. Dawa si kuwatawanya, ni kuwasikiza.