Makala

TAHARIRI: Serikali kupungukiwa na hela ni hatari kuu

March 8th, 2018 1 min read

Na MHARIRI

MATAMSHI ya Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich kwamba serikali haina fedha Za kutosha kugharimia miradi yake hapa nchini ni fedheha na hatari zaidi kwa wananchi wa taifa hili.

Akihojiwa mbele ya kamati ya seneti inayosimamia bajeti na fedha, Waziri huyo alisema kwamba kipindi kirefu cha kupinga uchaguzi kuliathiri nchi kiuchumi, hivyo basi akatangaza kuwa analenga kupunguza mgao unaotengewa kaunti 47 kutoka Sh302 bilioni hadi Sh285 bilioni.

Mwanzo ni kinaya kwamba serikali imedidimia kifedha ilhali baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa miaka ya nyuma kupunguza gharama ya matumizi hayajatekelezwa.

Baadhi ya mapendekezo hayo ambayo haijabainika kama yalitekelezwa, ni kupunguzwa kwa mshahara wa Rais,naibu wake na maafisa wa ngazi za juu serikalini mapema mwaka wa 2014.

Viongozi wetu wanaohudumu bungeni walipoona pendekezo la Tume ya Mishahara nchini (SRC) kupunguza mshahara wao walifanya kila juhudi kuhakikisha kwamba hilo halitimii.

Wakati wa mjadala huo bungeni, tofauti za mirengo zilitupwa kando na kuhakikisha kuwa maslahi yao yanadumishwa.

Waziri anapotaja kwamba Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) imefeli kufikia viwango lengwa ina maana kuna nia fiche ya kuongeza kodi ama kuhakikisha mabwenyenye wanaokwepa kutozwa ushuru wanakabiliwa.

Lakini suala zito linalofaa kuzingatiwa baada ya waziri huyo kutangaza hayo ni, je,serikali za kaunti zitatumia mbinu zipi kuhakisha kwamba pengo hilo la hela linazibwa? Iwapo hamna chochote kitakachofanyika, basi huenda kaunti zikajipata kwenye matatizo chungu nzima.

Tamko hilo la Bw Rotich linahofisha zaidi kwa sababu nchi ambayo haiwezi kumudu gharama ya huduma kwa raia wake ndiyo hukimbilia mikopo kiholela.

Kwa sasa nchi tayari inakumbwa na mgomo wa wahadhiri ambao wanataka mshahara zaidi kulingana na makubaliano ya mwaka jana. Je, hali ikiwa hivi watashughulikiwa kweli?.

Jambo la wazi kama mchana wa jua ni kwamba serikali haijaweka mikakati maridhawa ya kupunguza gharama yake na kulitokomeza kabisa donda sugu la ufisadi.