Makala

TAHARIRI: Serikali na KNUT wajali wanafunzi

December 31st, 2018 2 min read

NA MHARIRI

TANGAZO la chama cha walimu nchini (KNUT) kwamba kinapanga kuanza rasmi mgomo Alhamisi, linajiri wakati shule zinapotarajiwa kufunguliwa kwa muhula wa kwanza.

Kwenye barua kwa makatibu wa matawi yote ya chama hicho, Katibu Mkuu Wilson Sossion anawaagiza wahakikishe hakuna shule inayofunguliwa. Anadai kuwa kuna masuala manne ambayo chama hicho yanataka yajadiliwe na kutatuliwa, lakini hakuna dalili kuwa yatapata ufumbuzi.

Kwa muda wamekuwa wakizozana na mwajiri wao, TSC kuhusiana na masuala ambayo wanaamini yangeshughulikiwa kwa njia tofauti. Mojawapo ni uhamisho wa walimu wakuu kutoka maeneo yao hadi kwengine. Mpango huo umekuwa ukiendelea kwa muda sasa na KNUT inaamini kuwa unatatiza familia nyingi.

TSC kwa upande wake imekaza kamba na kusema kama mwajiri wa walimu, ina haki na uwezo kisheria kuamua kuhusu jinsi ya kuwasimamia walimu na utendakazi wao.

Walimu wana haki ya kikatiba kugoma, wanapohisi kuwa maslahi na matakwa yao hayatekelezwi. Wamekuwa wakitumia njia za kisheria kuitisha migomo siku za nyuma na hata safari hii wamefuata mkondo huo.

Lakini katika kuitisha migomo, maafisa wa KNUT wanapaswa kuzingatia kuwa kama ambavyo fahali wawili wanapokabiliana zinazoumia ni nyasi, masomo ya watoto huathiriwa.

Katikati ya mwezi huu, Waziri wa Leba, Bw Ukur Yattani aliteua jopo la kusikiza pande zote mbili na kuleta maelewano. Katika kumteua Bw Charles Maranga kuongoza jopo hilo, tunatumai waziri hajafanya kwa lengo la kisiasa. Masuala ambayo walimu katika nchi hii wameyaibua ni ya msingi na yanayostahili kushughulikiwa kwa njia ya ukomavu.

Wazazi nchini tayari wanakabiliwa na changamoto tele muhula mpya unapokaribia kuanza. Zawadi bora zaidi ya Mwaka Mpya kwao ni kutatua changamoto zinazohusiana na masuala ya elimu.

Wakenya wengi ni watu wa mapato ya chini na urathi pekee wanaoweza kuwapa watoto wao, ni elimu bora inatakayowasaidia siku za usoni. Hili ni jambo ambalo kila mdau kwenye mzozo kati ya walimu na mwajiri wao wanapaswa kulifahamu.

Wizara za Leba na Elimu pia zina wajibu wa kutilia mkazo umuhimu wa kupatikana suluhu katika mzozo unaoendelea. Elimu hutengewa mgao mkubwa wa fedha na mlipa ushuru, na wanaoisimamia hawana budi kutekeleza wajibu wao wakimjali zaidi mwanafunzi.