Makala

TAHARIRI: Serikali ni kizingiti kwa ukuaji wa spoti

October 26th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

UFAFANUZI wa Waziri wa Michezo Bi Amina Mohamed siku ya Alhamisi alipofika mbele ya kamati ya michezo ya Bunge la taifa kuhusu hatua zilizopigwa katika ujenzi wa viwanja nchini unatamausha.

Mnamo 2013 serikali ya Jubilee iliahidi kujenga viwanja vitano vya kisasa nchini kama hatua mojawapo ya kupiga jeki maendeleo ya michezo nchini.

Baada ya kuzembea na hivyo kufeli kutimiza ahadi hii kufikia uchaguzi uliofuata, serikali kama njia mojawapo ya kujiondolea aibu ikatangaza mnamo 2017 kwamba ingeongeza idadi ya viwanja hivyo hadi 11 na kwamba vingeshughulikiwa kwa dharura.

Hata hivyo, muhula wa pili wa serikali ya Jubilee sasa unakaribia kufika katikati ilhali hakuna matumaini kwamba ahadi hiyo ya kujengwa kwa viwanja 11 vipya itatimizwa.

Alipokuwa akihojiwa na wabunge, Waziri Mohamed alieleza kwamba ujenzi wa viwanja husika uko katika hatua mbalimbali za kati ya asilimia 15 na 75 kukamilika.

Waziri alilalamika kwamba chanzo kikuu cha kuchelewa kukamilishwa kwa ujenzi wa viwanja husika ni hatua ya wizara ya fedha kutotoa pesa zote inazotengea michezo katika bajeti ya kila mwaka.

Alielezea kufadhaishwa kwake na kutolewa kwa hata thuluthi moja pekee ya pesa ambazo hutengwa katika bajeti ya michezo.

Wakenya wengi wamekuwa wakishangaa ni kwa nini ahadi ya serikali iliyotolewa kuanzia 2013 imechukua muda mrefu kutekelezwa. Sasa ukweli umefichuliwa na Waziri Mohamed. Ufichuzi huu unafanya tuanze kutilia shaka uaminifu wa serikali katika utekelezaji wa ahadi zake. Inakera kuona serikali ikihadaa wananchi wake tena kwa macho makavu.

Hili si tukio la pekee ambapo serikali imewahadaa Wakenya kuhusu masuala ya spoti. Zaidi ya mwaka mmoja uliopita, serikali ilianza kutoza ushuru kampuni zote za kamari kwa ahadi ya kubuni hazina maalum ambayo ingetumiwa kupiga jeki spoti mbali na kugharimia matibabu pamoja na uhamasishaji kwa umma kuhusu athari za kamari nchini.

Licha ya hazina hiyo kuanzishwa na ushuru kutozwa, serikali haijatoa pesa zilizopatika kuwafaa wanaspoti. Mbali na kutojengwa kwa viwanja ilivyoahidi, serikali haijawahi kueleza zilikoenda hela zilizokusanywa kutoka kwa kampuni za kamari; hela ambazo zilikuwa ziwekezwe katika michezo. Ni aibu serikali kuhadaa raia wake.