TAHARIRI: Serikali yafaa irahisishe harakati ya kuingia Gredi 7

TAHARIRI: Serikali yafaa irahisishe harakati ya kuingia Gredi 7

NA MHARIRI

JUMA lijalo, wanafunzi wa Gredi ya 7 wanatarajiwa kujiunga na shule mbalimbali kwa masomo ya Sekondari ya Msingi chini ya mtaala mpya wa elimu almaarufu CBC.

Hili ndilo darasa la kwanza kabisa chini ya Mtaala wa Umilisi (CBC).

Kutokana na hali hiyo, pana sintofahamu kubwa hasa kuhusu shule watakazojiunga nazo wanafunzi hao.

Tatizo hilo linazuliwa na baadhi ya shule kukosa kutimiza masharti ya kuanzisha kitengo cha sekondari katika shule za msingi.

Hiyo ina maana kuwa wanafunzi watakaoathiriwa na masharti hayo watahitajika kutafuta shule za msingi zilizo na kitengo cha sekondari ya msingi.

Wanafunzi hao watahitajika ama kutafuta nafasi ya kujiunga na daraja hiyo ya elimu katika shule za mbali au kuhamia katika shule zinazotoza karo ya juu kuliko uwezo wa wazazi.

Huenda wanafunzi wengi wakasusia shule kutokana na mwendo mrefu watakaohitajika kusafiri ili kufikia shule zao mpya. Kunao watakaosoma kwa taabu kutokana na umbali huo.

Pia itakuwapo changamoto ya usalama kutokana na umbali ambao mwanafunzi atahitajika kusafiri; hasa wanafunzi wanaotoka katika maeneo yanayofahamika kwa mizozo.

Kwa wanafunzi wa shule za mijini, idadi ya wanafunzi wa Gredi ya 7 inatarajiwa kupanda zaidi kutokana na uchache wa shule zinazofuzu kutoa elimu ya sekondari hiyo ya msingi.

Wingi wa wanafunzi madarasani utazua changamoto ya ufundishaji ambapo itakuwa vigumu kwa walimu kuwafunza wanafunzi wengi kupita kiasi.

Aidha, shule hizo zitalazimika kuongeza karo kwa sababu ya hitaji la walimu wengi, madarasa zaidi na walimu.

Ikizingatiwa kuwa uchumi wa nchi umevurugika, itawawia vigumu wazazi au walezi wengi kumudu karo ya juu; hali ambayo inaweza kulazimisha watoto wengi kusalia makwao na kukosa elimu.

Changamoto hizi ni miongoni mwa nyingine nyingi zinazokabili utekelezaji wa mfumo wa CBC. Hata hivyo, muhimu zaidi kwa sasa ni kulivuka daraja tunapofikia.

Njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto hizi ni kuhakikisha kuwa shule nyingi zimewezeshwa kutimiza masharti ya kufanikisha masomo ya Gredi ya 7, 8 na 9.

Serikali pia inafaa izisaidie shule zinazowasajili wanafunzi wa Gredi ya 7 kwa njia mbalimbali kama vile kuzipa walimu wa kutosha, kuzisaidia kujenga madarasa zaidi, maabara na maktaba zinazokidhi mahitaji ya wanafunzi watakaojiunga na taasisi hizo.

Vinginevyo, azimio la kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu ya msingi halitatimizwa.

  • Tags

You can share this post!

Wafuasi njiapanda Raila akikana Ruto

CECIL ODONGO: Ruto, Gachagua polepole wanaingia mtego wa...

T L