Michezo

TAHARIRI: Sharti kocha mpya athibitishe ufaafu

August 17th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) lafaa liwadhihirishie Wakenya kuwa kocha mpya wa timu ya taifa Harambee Stars ana uwezo wa kuifikisha timu hiyo mbali hata ikiwezekana katika fainali za Kombe la Dunia la 2022 litakalofanyika nchini Qatar.

Aidha, ni muhimu kocha anayemrithi kocha Sebastien Migne ajifunze kutokana na makosa ya mtangulizi wake huyo hasa yaliyofanyika katika fainali za Kombe la Afrika (AFCON) na kabumbu ya kufuzu kwa fainali za Ubingwa wa Afrika (CHAN).

Baadhi ya makosa ya Migne yalikuwa kuteua kikosi kiholela, kupanga wanasoka uwanjani bila busara na mtindo mbovu wa kukabiliana na timu stadi kama vile Senegal na Algeria katika fainali za Kombe la Afrika zilizokamilika mwezi jana nchini Misri.

Kocha mzoefu Francis Kimanzi aliyekuwa msaidizi wa Migne ndiye anayepewa mikoba ya Harambee Stars.

Hii si mara ya kwanza kwa mkufunzi huyo wa klabu ya Mathare United kupewa usukani wa Harambee, amewahi kuifunza timu hiyo ya taifa.

Maadamu anasaidiwa na mjuzi mwenzake Zedekiah ‘Zico’ Otieno, ambaye pia amewahi kushikilia hatamu kama kocha wa Harambee, mashabiki wanatarajia mambo makuu wala si masihara ambayo timu hii imefanyiwa.

Inaaminika kuwa iwapo Migne angekabiliana na Algeria na Senegal kwa kujiamini, Kenya haingeaibishwa jinsi ilivyofanyiwa Misri. Ilikuwa bayana kuwa Harambee iliwaogopa kabisa Senegal na Algeria, ndiyo maana ikaamua kucheza mchezo wa kuzuia pekee.

Mataifa kama Uganda ambayo yalijiamini, yalitatiza sana timu kubwa mbali na kwamba mchezo wake uliridhisha wengi.

Katika fainali za 2004 nchini Tunisia, chini ya kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee, Kenya hasa ililemewa kutokana na kukosa kuchezesha wanasoka wanaoelewana uwanjani, mathalani ushirikiano baina ya Dennis Oliech na John Baraza ulikosekana katika mechi mbili za kwanza.

Katika mechi hizo Kenya ilitandikwa kiaibu.

Hivyo basi ni muhimu Kimanzi na Zico wajifunze kutokana na makosa hayo.

Wasichezeshe vijana mchezo wa kuogopa, wasiteue kikosi kwa mapendeleo na ubinafsi na wawe waangalifu katika kufuatilia mchezo wa wanasoka katika ngazi ya klabu.

Nayo Serikali sharti isaidie Harambee Stars kifedha na katika kukuza mchezo kuanzia mashinani pamoja na kuimarisha miundomsingi. Itakuwa aula iwapo vipawa vitaanza kutambuliwa na kunolewa mapema.