Makala

TAHARIRI: Sheria kali kuhusu noti mpya zikazwe

June 6th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

Hatua ya serikali kutangaza siku ya kuharamisha noti ya sasa ya Sh1,000 ni ya kupendeza ila ina walakini moja.

Muda uliowekwa kama makataa ya amri hiyo ni mrefu kiasi kwamba huenda wanaonufaika kutokana na pesa haramu walizoficha majumbani mwao wakapata mwanya wa kuzibadilisha haraka haraka na hivyo kuendelea kunufaika na mali ya kilaghai.

Inapozingatiwa kuwa mamilioni ya Wakenya wanateseka hasa kutokana na watu wenye hila kuficha pesa zao haramu majumbani, inakuwa bora wahusika wakumbane na ugumu katika harakati ya kutii amri hiyo ya serikali. Na ugumu huo utajitokeza vizuri iwapo muda wa kubadilisha noti hizo utafupishwa.

Baadhi ya wabunge, hasa wa chama cha ODM walipendekeza kuwa muda huo ufupishwe hadi Agosti 1 badala ya Oktoba 1, nasi twawaunga mkono.

Maadamu wengi walioficha pesa hizo ni watu wenye uwezo na mamlaka pamoja na ushawishi, wanapopewa muda mrefu wa kutii agizo hilo, wanaweza kubuni mbinu mbalimbali za kubadilisha pesa zao na hivyo basi kuendeleza hali ya sasa ya kiuchumi inayowatatiza wengi.

Kauli hii haimaanishi kuwa kila aliyeweka pesa nyingi nyumbani kwake alizipata kwa njia ya kutiliwa shaka; la. Wapo wananchi, japo wachache ambao walitolea jasho pesa zao.

Lakini wengi ni walioiba mali ya umma na kuificha kwa sababu wanaogopa kuwa wakiipeleka kwenye benki, ni rahisi mkono mrefu wa serikali kuwafikia.

Kadhalika, kutokana na manufaa maridhawa ya hatua hiyo ya serikali, pana haja ya kubuni kanuni kali zitakazowazuia watu hao laghai kubadilisha pesa hizo.

Naam, tayari serikali imebuni sheria kadhaa, mathalani kuhusu kiwango cha pesa kinachoweza kubadilishwa katika benki za kawaida na benki kuu (CBK) pamoja na afisi za kubadilisha pesa za kigeni.

Hata hivyo, ipo mianya inayoweza kutumiwa na watu hao fisadi kubadilisha pesa hizo. Mianya hiyo ndiyo inayofaa kugunduliwa upesi na kuzuiwa.

Mbali na kwamba hatua hiyo ya serikali ni muhimu kwa kuwa italainisha uchumi wa Kenya hasa kwa sababu pesa zitaanza kusambaa tena na hivyo kupiga jeki shughuli za kibiashara na uwekezaji, Mkenya wa kawaida ataanza kuhisi nafuu kwani msambao huo wa pesa utamfikia na kumnufaisha. Kwa hivyo, ni muhimu amri hiyo ya serikali izingatiwe kwa uangalifu mkuu.