Makala

TAHARIRI: Sheria kuhusu Naibu Gavana irekebishwe

April 25th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

WIKI hii Bunge la Seneti limemhoji Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuhusu madai kuwa amekaidi ushauri wa Mahakama ya Juu kwa kuendesha serikali bila naibu gavana.

Maseneta walitaka kujua ni kwa nini gavana huyo ameendesha serikali ya kaunti yake kwa miezi 15 bila ya naibu, tangu alipojiuzulu Bw Polycarp Igathe.

Sababu ya kumwita ni kuwa mwenzake wa Nyeri, Mutahi Kahiga aliupa uzito ushauri wa Mahakama ya Juu na akamteua naibu wake mara moja.

Kamati hiyo ya Ugatuzi inayoongozwa na Seneta wa Laikipia, Bw John Kinyua, pia ilimtaka aeleze kwa nini amekuwa akifanya kazi na mawaziri watano pekee.

Kwanza, yafaa tukubaliane na Bw Sonko kwamba hakuna sheria inayomlazimu gavana kumteua naibu wake. Sheria kuhusu Usimamizi wa Serikali za Kaunti haimshurutishi kuteua naibu wake wala kufanya kazi na idadi kamili ya mawaziri.

Ushauri wa Mahakama ya Juu haukuwa amri kwamba lazima gavana ateue naibu wake na wala hakuna kipengee chochote cha sheria kinachowaamrisha magavana kuteua manaibu wao baada ya kipindi fulani.

Japokuwa sheria kuhusu Ugavana ilijaribu kukopa kutoka ile ya urais, haijafafanua mambo mengi kuhusu wadhifa ambao mara nyingi unashikiliwa na watu wasiokuwa na majukumu maalumu.

Kinyume na Naibu Rais ambaye hupewa majukumu ya mara kwa mara na rais, naibu wa gavana anakuwa mtu ambaye utendakazi wake unategemea kama anasikizana na gavana au la.

Maseneta walikubaliana na Bw Sonko kwamba kuna sheria inayosubiri kupitishwa, itakayoeleza mambo hayo kwa kina. Hata hivyo, ni mtazamo wetu kuwa wadhifa wa Naibu gavana wafaa kujumuishwa kwenye zile nyadhifa za uongozi wa umma zinazofaa kuangaliwa upya iwapo kutakuja marekebisho ya Katiba.

Gavana Sonko amedhihirisha kuwa afisi ya gavana inaweza kutekeleza majukumu yake bila ya kuwa na msaidizi. Iwapo ni lazima nafasi hiyo iendelee kuwa, basi kuna haja ya kurekebisha sheria ili manaibu wa magavana wapewe majukumu maalumu yenye manufaa kwa wananchi.

Majukumu hayo, hayafai kuonekana kama yanayompunguzia gavana mamlaka ya kutekeleza kazi aliyopewa katika kusimamia kaunti. Migongano ya aina yoyote katika majukumu ya wawili hao, itasababisha uongozi mbaya.