TAHARIRI: Sheria yafaa ibadilishwe mshindi wa uchaguzi abainike upesi

TAHARIRI: Sheria yafaa ibadilishwe mshindi wa uchaguzi abainike upesi

NA MHARIRI

KUNA haja kubwa ya sheria ya uchaguzi kubadilishwa ili mshindi aweze kubainika upesi.

Hii ni kutokana na hali ya shinikizo, taharuki, mihemko na hata habari potoshi, ambayo imeshuhudiwa miongoni mwa Wakenya katika siku tatu za kwanza baada ya uchaguzi mkuu wa Jumanne.

Katika muda wa siku hizo tatu, Wakenya wengi walishindwa kulala au kuendelea na shughuli zao kutokana na mawazo yao kuelekezwa kwa ni nani atakayeshinda kati ya Raila Odinga wa Azimio la Umoja na William Ruto wa Kenya Kwanza (UDA).

Hili lilidhihirika kupitia simu nyingi zilizopigwa na Wakenya wengi kuulizia ni nani aliyeshinda huku upotoshi mwingi ukizagaa katika mitandao ya kijamii kuhusu aliyekitwaa kiti cha urais.

Hayo si mazingira mazuri ya kujipata kwayo maadamu kwa hakika yana athari mbovu za kiafya kutokana na msongo wa mawazo.

Kwa sababu hiyo, twafaa tuige mifumo ya mataifa kama vile Amerika ambayo saa kadhaa baada ya shughuli ya upigaji kura kukamilika, mshindi huanza kujulikana.

Katika enzi hii ya kidijitali, sheria ya Mahakama ya Juu kuwa sharti nakala za karatasi ziwasilishwe kutoka vituo vya eneobunge vya kujumlisha matokeo ya kura, ndipo tume ya uchaguzi ianze kupiga hesabu, hakika ina utata.

Ingawa sharti hilo liliwekwa ili kuhakikisha kuwa hakuna udanganyifu unaotokea kutokana na upeperushaji wa matokeo ya kidijitali, itakuwa bora njia mbadala ipatikane ili kuhakikisha matokeo yanayopeperushwa hayabadilishwi na watu wenye nia mbaya, na hivyo basi kusaidia kuondoa dukuduku mioyoni mwa Wakenya linalotokana na kucheleweshwa kwa matokeo.

Hali ilivyo kwa sasa, IEBC haina ruhusa ya kupeperusha matokeo moja kwa moja kutokana na sababu kuwa sharti ipakue Fomu 34A ambazo ni nyingi mno (zaidi ya 46,000) kisha inakili kando ndipo ijumuishe na kupeperusha matokeo yake.

Kwa hivyo, kwa kuwa shughuli hiyo ni ngumu, vyombo vya habari ndivyo vilivyopewa ruhusa ya kujumlisha hesabu na kupeperusha matokeo yake ambayo si rasmi.

Hatimaye fomu za karatasi zinapowasilishwa, kwa IEBC hasa zile za jumla ya kura za kila eneobunge (Form 34B), ndipo tume hiyo huanza kujumlisha na kupeperusha matokeo yake.

Huwa yamechelewa sana na kuwaumiza wananchi.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Sheria ikazwe kuadhibu wanaoeneza matokeo...

WANDERI KAMAU: Teknolojia ya uchaguzi IEBC ingefanywa na...

T L