TAHARIRI: Suluhu ya haraka itafutwe kuhusu marufuku ya mabasi ya shule

TAHARIRI: Suluhu ya haraka itafutwe kuhusu marufuku ya mabasi ya shule

KITENGO cha UHARIRI

AGIZO kutoka kwa waziri wa Elimu nchini Profesa George Magoha kuhusiana na utumizi wa mabasi ya shule huenda likazorotesha uhusiano bora uliopo kati ya usimamizi wa shule na wazazi.

Kwenye agizo lake waziri Magoha aliamuru wanaotaka kutumia mabasi ya shule wapate kibali maalum kutoka kwa Wizara ya Elimu wala si mwalimu mkuu wa shule kama ilivyo kuwa ada hapo awali.

Ingawa agizo hilo halikufafanua waziwazi kuhusu jinsi ya kupata vibali hivyo maalum, ni wazi kwamba mabadiliko hayo ya ghafla yalilenga kupiga marufuku wazazi kutumia magari hayo kutoka kwa walimu wakuu kama ilivyokuwa zamani.

Bila shaka Prof Magoha huenda ana sababu nzuri za kutoa agizo hilo ila huenda likawa na athari zisizotamanika kwenye mahusiano ya wazazi na Bodi ya Kusimamia Shule. Awali wazazi walikuwa wakikubaliwa kukodisha mabasi ya shule kwa bei nafuu ikilinganishwa na magari ya usafiri wa umma.

Wazazi walihakikishiwa usafiri bora na pia usalama wa kiwango cha juu kwa sababu mabasi ya shule aghalabu huwa yamedumishwa na kuwekwa kwa hali bora kila wakati. Zaidi ya hayo, madereva wake huwa wenye nidhamu ya hali ya juu, hivyo huwa waangalifu kuliko madereva wa matatu.

Nazo shule huwa zinafaidika si haba kwani vijifedha ambavyo zinapata huweza kupiga jeki uendeshaji miradi kama ujenzi, ulipaji mishahara ya wafanyakazi wao au hata kununua vifaa wakati ulipaji karo unapokwama kutokana na hali mbaya ya kiuchumi hasa kipindi cha gonjwa hatari la Covid.

Sio hivyo tu, mabasi haya huhitaji gharama ya kuyaweka katika hali bora kila baada ya matumizi ya muda fulani. Fedha hizi huwa zinafaa shule kusimamia hitaji hili bali na kulipia deni endapo basi husika lilinunuliwa kwa kiasi fulani cha mkopo.

Si ajabu kwamba hata mabasi ya makanisa hukodishiwa na wazazi na waumini, bora kiwango cha nidhamu cha wanaoikodisha kiwe cha kukubalika.Kwa kuzingatia haya, waziri wa Elimu anafaa kurejelea msimamo wake na pengine kuuangaliwa upya la sivyo wazazi huenda wakaanza kurukia walimu na maafisa wa wizara ya Elimu.

Ikumbukwe kuwa kuna baadhi ya wazazi waliochangia katika ununuzi wa mabasi haya. Suluhisho la haraka linafaa kusakwa kwani tayari baadhi ya wazazi wameanza kunung’unika kuwa maafisa wa Elimu wanawanyima mabasi ya shule

You can share this post!

Wavamizi waua polisi, wateka Wachina 5 kambini

Maji tele Pwani lakini nyumba zakosa tone!

T L