TAHARIRI: Suluhu yahitajika shule za sekondari

TAHARIRI: Suluhu yahitajika shule za sekondari

KITENGO CHA UHARIRI

SHULE za Upili kote nchini zinatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza wiki ijayo kuanzia Agosti 2 na 6.

Idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kwa jumla ni 1.1 milioni.

Wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na shule za kitaifa ni 33,009, huku 184,816 wakielekea katika shule za kaunti kiwango cha juu (Extra County).

Wengine wapatao 188,454 wameratibiwa kusajiliwa katika shule za kaunti na wenzao 669,145 wakipelekwa katika shule za kaunti ndogo.

Huku maandalizi ya kuwapokea watoto hawa yakiendelea, walimu wakuu huenda wakajipata katika hali ya suitafahamu kuhusu namna ya kumudu idadi hii kubwa ya wnafunzi katika mwaka huu mfupi zaidi wa masomo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ni wanafunzi 747,161 waliomaliza masomo ya Kidato cha Nne mwaka wa masomo uliopita, hivyo basi kumaanisha kuwa nafasi zilizo tayari kuchukuliwa wanafunzi wapya kote nchini ni takriban 400, 000 pekee.

Kutokana na takwimu hizi, wasimamizi wa taasisi hizi watahitajika kupanua huduma zao hili kusitiri idadi hii kubwa ya wanafunzi mwaka huu. Bila shaka itawabidi wapanue madarasa, bweni, maabara, maktaba na hata idadi ya walimu wataowashughulikia wanafunzi hawa.

Suala hili huenda likageuka mzigo kwa walimu wakuu kwa kuwa upanuzi huu unahitaji fedha nyingi kuwawezesha kufikia lengo hili kikamilifu.

Hitaji la walimu ni la lazima kwa kuwa idadi wa walimu nchini haitoshelezi idadi ya wanafunzi waliokuwepo kabla ya ongezeko hili.

Miaka mitatu iliyopita, ongezeko kubwa la wanafunzi lilishuhudiwa baada elimu ya sekondari kuwa ya lazima kisheria nchini.

Upungufu wa vifaa vya wanafunzi ulishuhudiwa pakubwa. Hata ingawa Serikali ilichangia kifedha kupiga jeki juhudi za kupanua shule, bado utoshelezaji uliolengwa haukufikiwa.

Ongezeko zaidi kama inavyoshuhudiwa sasa inaongezea walimu wakuu majanga zaidi.

Suala la janga la corona ndilo linalozihangaisha zaidi Bodi za Usimamizi za shule hizi (BOM) kwa kuwa masharti ya kudumisha umbali na usafi ndiyo msingi hakika wa kukabiliana na msambao wa maambukizi ya corona ndani ya taasisi.

Bodi hizi zina majukumu mazito ya kuhakikisha fedha zimepatikana kwa dharura kupanua shule ili kutoa elimu bora kwa wasomaji hawa wachanga.

Ukabilianaji wa suala hili si mzaha bali unawahitaji wajitolee mhanga.

Ili kufikia lengo hili, serikali za kaunti na ile kuu zinafaa kujifunga kibwebwe kuhakikisha shule zimepata ufadhili wa kutosha kutekeleza upanuzi kulingana na idadi ya wanafunzi husika.

Kutokana na hali mbaya ya uchumi, wazazi hawafai kuongezewa madhila ya kifedha kwa kuwa hata ulipaji wa kiwango cha karo cha sasa kwao ni mzigo usiobebeka.

Serikali itimize ahadi yake ya kutoa elimu ya lazima kwa kilz mtoto wake bila kusita

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Matunda ya elimu yamsukuma kuwa mtetezi sugu...

ODONGO: Mudavadi na Kalonzo hawawezi kitu bila Raila