TAHARIRI: Taifa liige Kilifi kukabili mimba za mapema

TAHARIRI: Taifa liige Kilifi kukabili mimba za mapema

KITENGO cha UHARIRI

MNAMO 2018, kaunti ya Kilifi iligonga vichwa vya habari wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya mitihani ya kitaifa kutokana na kurekodi visa vingi zaidi nchini vya watoto wasichana kupata mimba na hivyo kukatiziwa masomo.

Wakati huo, Kilifi ilirekodi asilimia 33 ya vijana ambao walipata mimba za mapema. Tangu mwaka huo hadi sasa, visa vya mimba za mapema vimekuwa vikipungua kila mwaka hadi kufikia sasa ambapo vimefikia asilimia 13.

Nyingi za mimba za mapema miongoni mwa vijana zilitokana na ukosefu wa elimu kuhusu masuala ya uzazi pamoja na umaskini. Wengi wa wasichana waliungama kushiriki ngono na watu wazima hasa wanaume walifanya kazi ya bodaboda ili waweze kupata hela za kukimu mahitaji msingi kama vile chakula na sodo.

Kutokana na hatari iliyokodolea macho kaunti ya Kilifi na kuangaziwa katika vyombo vya habari, serikali ya kitaifa na ile ya Kaunti zilichukua hatua. Mathalan, makundi ya marika yalianzishwa. Katika makundi haya, mabinti waliopata watoto walisaidiwa kwa malezi huku wakipewa mafunzo kuhusu ngono salama pamoja na mbimu mbalimbali za kupanga uzazi.

hatua hii ililenga kuwapunguzia shinikizo na pia kuwahami na elimu ya kuwatoa katika hadaa na hatari za ngono. Wengi wa mabinti hawa walirejea shuleni na kuanzisha makundi ya kuwahamasisha wasichana wenzao.

Chanzo kingine cha mimba za mapema kilikuwa disko matanga, hizi pia zilipigwa marufuku na serikali.Hatua hizi zote za serikali zimenusuru mabinti wengi na sasa mimba za mapema zimepungua na hivyo kuwawezesha mabinti kuendeleza masomo.

Maadamu visa vya mimba za mapema zimezagaa kote nchini, kaunti na taifa kwa ujumla linafaa liige mfano huu kama njia mojawapo ya kuwaokoa wasichana wetu.

You can share this post!

Njaa yawakosesha wanafunzi 1,603 umakinifu Mbeere

JAMVI: Bado sijaanza kampeni za 2022 – Ruto

T L