Makala

TAHARIRI: Tuambiwe ukweli wa ziara ya Somalia

March 3rd, 2020 2 min read

Na MHARIRI

KAULI ya wabunge wa eneo la Kaskazini mwa Kenya kwamba walienda Somalia kwa nia njema, yafaa kutiliwa shaka na kila raia anayependa uthabiti wa nchi yetu.

Wabunge hao 11 japo walinaswa Jumapili jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi wakitoka Somalia, waliachiliwa bila ya kufunguliwa mashtaka yoyote.

Ziara yao Somalia inasemekana kuwa ilifanywa bila idhini kutoka kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni wala Spika wa Bunge Justin Muturi, kama inavyohitajika kisheria.

Mmoja wao alidai kuwa wakiwa Somalia, walikutana na Rais wa Somaliland, Bw Mohamed Abdullahi Farmajoo pekee. Eti miongoni mwa masuala mengine, walimtaka akome kuandika barua za matusi dhidi ya Kenya.

Kauli ya wabunge hao na hata maafisa wa ujasusi wa Kenya ni ya kutiliwa shaka. Kama kweli wabunge hao walienda huko bila ya serikali yetu kuwa na habari, basi kunaibuka maswali mengi kuhusu usalama wetu.

Itakuwaje waliabiri ndege na kuondoka bila ya mtu yeyote katika uwanja wa ndege au idara ya Uhamiaji kuwa na habari? Kama raia wetu, ambao ni viongozi wanaojulikana, wanaweza kuondoka nchini bila ya mtu kuwa na habari, ni wageni wangapi hatari wanaoweza kuingia wasijulikane?

Kenya, tunatambuliwa kwa kuwa na vikosi imara vya ujasusi. Maafisa wetu wamepata mafunzo ya hali ya juu katika mataifa kama vile Israel. Kutangazia ulimwengu mzima kuwa hakuna aliyekuwa na habari, ni uongo au kukiri kuwa hatuna ulinzi tena.

Kuanza kuuliza nia ya wabunge hao, ilhali kuna sheria zilizowekwa kuhusu hatua anazopaswa kuchukua mbunge kabla ya kwenda nje ya nchi, ni kuhadaa Wakenya au kukiri kuwa siku hizi sheria ni ya mtu mdogo pekee.

Kama kweli wabunge hao walikuwa wanaenda Somalia kuzungumza na Bw Farmajoo kwa niaba ya Kenya, nani aliwatuma? Ni kwa nini hawakuandamana na afisa yeyote wa ubalozi, usalama au ujasusi ili kufahamu kilichozungumzwa?

Ilisemekana kuwa waliabiri ndege ya Salaamair Air Express Flight WU-751 hadi mjini Mogadishu, Somalia. Huu ni ushahidi kamili kuwa yupo aliyewaona wakienda. Kama kweli waliondoka bila idhini, basi mbona hawajashtakiwa kwa kuvunja sheria?

Japokuwa ni hamu ya kila Mkenya kuona usalama umerejea nchini kwa kukabiliwa makundi ya kigaidi, ni sharti juhudi za kutimiza hilo zifanywe kwa uwazi na kufuata sheria.