Makala

TAHARIRI: Tuangalie mazuri ndani ya BBI

October 23rd, 2020 2 min read

Na MHARIRI

KUZINDULIWA kwa ripoti ya Maridhiano (BBI) sasa kunatoa fursa kwa Wakenya kuipitia kwa makini na kutoa tathmini yao kabla ya kufanya uamuzi.

Kwa kuaingalia kwa juu juu, ripoti hiyo inapendekeza mambo mengi yatakayokuwa ya manufaa kwa wananchi. Tangu Katiba ipitishwe Agosti 27,2010, kitu kikubwa ambacho wananchi wamekiona kuwa cha kuwafaa ni kutekelezwa kwa sura kuhusu Ugatuzi. Kuanzia mwaka 2013, Wakenya wamekuwa na magavana na watu wanajiamulia mambo yao wakiwa mashinani, bila ya kilio cha “Serikali Saidia”.

Huu ni mwelekeo ambao BBI sasa imeutilia nguvu. Kwanza, inapandisha kiwango cha chini cha pesa za kupelekwa kwa kaunti kutoka asilimia 15 hadi 35. Ina maana kwamba, kwa kila Sh100 ambazo nchi hupata, Sh15 zimekuwa zikitumwa kwa kaunti. Sasa BBI ikipitishwa, kaunti zitapata Sh35 kwa kila 100.

Kwenye pesa hizo, kila wadi itapelekewa pesa za kufanya maendeleo, sawa na ilivyo kwa wabunge. Kila mbunge hupewa pesa za kuendeleza eneobunge lake, zamani hazina hiyo ikijulikana kama CDF.

Watu katika kila wadi nchini, watakuwa na sababu ya kuitisha miradi kutoka kwa MCA wao, kwa sababu atakuwa akisimamia hazina maalumu kwa ajili yao.

BBI pia inapendekeza kuwe na Tume maalumu ya kusimamia madaktari na wahudumu wengine wa afya. Tume hiyo itakuwa sawa na ile ya walimu (TSC). Itafuatilia utendakazi wa wahudumu wa afya na kuwafanya wawajibike zaidi kuwashughulikia wagonjwa, bila ya kujali kama watakosa mishahara.

Vijana na wanawake watakaokopa pesa za kufanyia biashara watapewa miaka saba ya kujipanga, kabla ya kuanza kutakiwa walipe.

Haya ni mambo mazuri ambayo hayana uhusiano wowote na atakayekuwa Rais, Wairi Mkuu na Manaibu wa Waziri Mkuu.

Mwananchi atakapojisomea, anapaswa ajiulize kama tangu kwa mfano eneo anakotoka limekuwa na Rais, Naibu Rais au Waziri, amenufaika moja kwa moja sawa na inavyopendekezwa kwenye BBI.

Jambo pekee linalostahili kuangaliwa kwa makini, ni BBI kukosa kuifanya Seneti kuwa yenye kauli ya mwisho kuhusu masuala ya ugatuzi. Kisheria, maseneta ndio wasimamizi wa pesa za Kaunti. Itafaa kama watapewa nguvu kama nyumba yenye mamlaka kuliko Bunge la Taifa.