TAHARIRI: Tubadili mtindo wa kudumisha amani uchaguzi unapokaribia

TAHARIRI: Tubadili mtindo wa kudumisha amani uchaguzi unapokaribia

NA MHARIRI

HUKU Kenya inapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao ulioratibiwa kufanyika Agosti, mojawapo ya masuala makuu yanayoendelea kujitokeza ni kuhusu hitaji la amani.

Hili ni suala ambalo limekuwa likiibuka kila mara uchaguzi unapokaribia.

Mashirika ya serikali na yale yasiyo ya kiserikali huwekeza mamilioni ya pesa katika kipindi chote cha uchaguzi kuhamasisha umma kuhusu hitaji la kudumisha amani na kuepuka uchochezi wa wanasiasa.

Hata hivyo, wakati umefika sasa kwa wadau hao wote kutafakari kuhusu kwa nini juhudi hizi huwa hazizai matunda kwa kiwango cha kutosha. Hutakosa ghasia hapa na pale kila wakati wa kampeni au uchaguzi unapofanywa na hata baadaye.

Wadau wanaohusika katika kuhamasisha umma kuhusu amani wanafaa kutambua na kukubali ukweli kuwa tatizo kuu la uhasama humu nchini haliko kwa raia bali kwa viongozi wa kisiasa.

Hii ni mojawapo ya sababu zinazofanya Wakenya wa makabila na matabaka tofauti wawe wakiishi kwa umoja na amani kwa miaka minne bila matatizo yoyote, lakini ifikapo wakati wa uchaguzi, utakuta jirani akimgeuka mwenzake na kuanza kumshambulia.

Macho yanafaa kuelekezwa kwa wanasiasa ili wao ndio warekebishe mienendo yao ikiwa kweli mashirika ya serikali na yale ya kutetea haki za raia yamejitolea kurekebisha hali hii.

Inafahamika kuwa kuna idadi kubwa ya wanasiasa ambao ni wabinafsi, hawajali kuhusu maslahi ya umma bali wanachotaka ni kuingia mamlakani kwa njia yoyote ile ili wajinufaishe pamoja na familia na wandani wao wa karibu.

Hatuwezi kushinda tukihubiria umma kuhusu mambo yale yale tuliyohubiri miongo iliyopita yakashindwa kuleta utulivu wakati siasa zinaponoga kwa hivyo ni lazima mbinu mpya zitafutwe.

Kwa sasa, sheria ambazo zimepitishwa kujaribu kudhibiti wanasiasa wachochezi wanaopenda kugawanya nchi hazijafanikiwa kuleta afueni.

Hii ni kwa sababu sheria hizo ni dhaifu, na wanasiasa wanaotegemewa kuzifanya ziwe na nguvu kupitia kwa bunge la taifa hawana haja kufanya hivyo kwa vile wanajijua. Wao ndio huenda wakawa mstari wa mbele kupitia adhabu watakazopitisha.

Hivyo basi, hata kama wadau wataendelea kuhamasisha umma kuepuka viongozi wachochezi, hatua zitafutwe kukabiliana na wachochezi hao ndipo tutaona mabadiliko kwa kiasi cha haja.

You can share this post!

Mulembe wapongeza Mudavadi, Weta’

Wanajeshi Burkina Faso wamzuilia Rais Kabore

T L