Makala

TAHARIRI: Tuboreshe usalama ili kuepuka uvamizi

January 6th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

MATUKIO ambapo wapiganaji wa al-Shabaab walifanya mashambulizi mawili Kaunti ya Lamu, yanapaswa kuchochea serikali kuimarisha usalama nchini.

Kwamba magaidi hao walikuwa na ujasiri wa kuvamia kambi ya kijeshi ambayo kwa kawaida huwa chini ya ulinzi mkali na kufaulu kuharibu vifaa vya kijeshi kunaonyesha kuwa wanaweza kupenya na kushambulia popote na wakati wowote.

Kabla ya kushambulia kambi ya jeshi jana katika kisiwa cha Manda, walikuwa wameshambulia mabasi kadhaa na kuua watatu watatu kabla ya maafisa wa usalama kuwasaka na kuua wanne.

Tunapongeza maafisa wa usalama kwa kuchukua hatua za haraka kuwaandama magaidi walioshambulia abiria wasiokuwa na hatia.

Tunapongeza vikosi vya usalama na maafisa wa ujasusi ambao mara kwa mara wamekuwa wakitibua njama za magaidi kutekeleza mashambulizi nchini.

Hata hivyo, wakati huu ambao ulimwengu uko katika tahadhari kufuatia tisho la Iran kushambulia vituo cha Amerika kulipiza kisasi kwa kuua Jemedari wake, kuna haja ya kuimarisha usalama na ukusanyaji wa habari za ujasusi.

Kupenya kwa magaidi hao mara mbili kaunti ya Lamu, kunaonyesha kwamba huenda kuna ulegevu katika mfumo wetu wa usalama na ushirikiano zaidi unahitajika miongoni mwa vitengo vinavyohusika.

Ikizingatiwa kwamba magaidi walishambulia kambi iliyokuwa na wanajeshi wa Amerika ni dhihirisho kwamba Iran haikuwa inafanya mzaha ilipoapa kulipiza kisasi.

Hivyo basi, kuna haja ya kuimarisha usalama hasa katika shule na taasisi za elimu, maeneo ya kuabudu, masoko, magari ya uchukuzi kama viwanja vya ndege, maeneo ya burudani yanayopendwa na watu wengi hasa wageni na watalii.

Hii ni kwa sababu magaidi wamewahi kulenga maeneo haya awali na kuua Wakenya. Makundi ya ugaidi yamekuwa yakibadilisha mbinu kila wakati kote tekinolojia inapobadilika na kila mmoja anajukumu la kupasha polisi habari anapopata habari zinazoweza kuhatarisha usalama wa Wakenya bila kusita.

Kufaulu kwa magaidi kutekeleza magaidi kunaweza kuathiri uchumi wa nchi na ni Wakenya watakaoumia. Vita dhidi ya ugaidi vinapaswa kuhusisha kila Mkenya kwa kusaidia serikali. Ikizingatiwa magaidi wamekuwa wakivuka mpaka kutoka Somalia kutekeleza mashambulizi, maafisa wa usalama wanapaswa kuimarisha doria mipakani.