Makala

TAHARIRI: Tuepuke refarenda yenye ubishi

November 20th, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

KUAHIRISHWA kwa hafla ya kuzindua ukusanyaji wa sahihi za kuunga mswada wa kura ya maamuzi kupitia mchakato wa maridhiano (BBI), kunafaa kutoa nafasi ya kujumuisha maoni ya makundi ya Wakenya ambao wameeleza kutoridhishwa kwao na mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

Kwamba hatua hiyo ilitangazwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na Naibu Wake William Ruto Jumatano, imetoa matumaini ya kuwepo kwa kura ya maamuzi isiyobishaniwa.

Dkt Ruto ni mmoja wa Wakenya ambao wameeleza kutoridhishwa kwao na mapendekezo ya ripoti hiyo miongoni mwa Wakenya wa matabaka mbali mbali.

Wengi wamekuwa wakiuliza kwa nini mchakato huo unaharakishwa na kufungia nje au kukataa maoni ya baadhi ya watu ilhali hawaipingi mbali wanachotaka ni mdahalo wa kitaifa wa kuimarisha ripoti hiyo.

Tunarudia kusema kuwa iwapo nia ya vinara wa mchakato huo, Rais Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ni kuunganisha Wakenya na kumaliza dhuluma za kihistoria, ukabila, ubaguzi na ufisadi, wanafaa kukumbatia maoni ya kila mmoja.

Kusikiliza maoni hakumaanishi kukubali yote. Hata hivyo hawafai kupuuza maoni mazuri kwa sababu yametolewa na mtu anayechukuliwa kuwa na msimamo tofauti mradi ni Mkenya.

Huu basi ndio wakati wa vinara hao kuthibitisha kwamba walikuwa na nia njema kuasisi mpango wa kubadilisha katiba. Kupuuza baadhi ya maoni ya watu kunaweza kufanya malengo ya mchakato huyo yasiafikiwe na kuletea nchi hasara na aibu.

Hasara kwa sababu pesa nyingi na muda mwingi umetumiwa kufikia sasa na wengi wameweka matumaini yao kwamba utabadilisha mwelekeo wa siasa na uongozi wa nchi hii na kuufanya kuwa bora zaidi.

Muda uwekwe wa mdahalo wa kitaifa kuhusu mapendekezo, sauti za wengi zizingatiwe na za wachache zinazofaidi wengi pia sizipuuzwe. Kama vile Rais Kenyatta huwa anawaambia Wakenya, nchi hii ni muhimu kuliko maslahi ya watu wachache.

Maslahi ya nchi yanafaa kuafikiwa iwapo sauti zao zinasikilizwa na kujumuishwa katika maamuzi muhimu ya kitaifa. Hivyo basi, hakuna maamuzi muhimu kama kubadilisha katiba.

Huu basi ni wakati mwingine wa Rais Kenyatta kuonyesha uongozi kwa kuhakikisha kura ya maamuzi haitapasua Kenya iwe kwa misingi ya kimaeneo, kisiasa au kijamii.