Makala

TAHARIRI: Tujifunze kutokana na makosa ya 2019

December 31st, 2019 2 min read

Na MHARIRI

TUMEINGIA siku ya mwisho ya 2019, mwaka ambao umekuwa wa mseto wa matukio; ya kujivunia na pia majanga.

Tunajivunia kuwa baada ya zaidi ya miaka 15, timu yetu ya soka Harambee Stars ilishiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Misri. Wasichana wetu – Harambee Starlets – walishinda kombe la Mataifa Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Ni mwaka ambapo Jaji Mumbi Ngugi alitoa uamuzi utakaoendelea kujadiliwa nchini hata mwaka ujao. Mnamo Julai 24, Jaji Ngugi aliamua kwamba magavana watakaokabiliwa na kesi za ufisadi watalazimika kukaa kando hadi kesi hizo zikamilike. Wa kwanza kuathiriwa na uamuzi huo alikuwa Gavana wa Samburu, Bw Moses Lenolkulal. Baadaye magavana Ferdinand Waititu (Kiambu) na Mike Sonko (Nairobi) walifuata mkondo huo.

Mnamo Oktoba 12, ulimwengu mzima ulisimama kwa saa mbili, kumtazama mwanariadha Eliud Kipchoge akivunja rekodi ya kukimbia marathon kwa Saa Moja na dakika 59.

Baada ya kusubiri kwa miezi mitatu, mnamo Novemba Wakenya walipewa matokeo ya Idadi ya Watu. Ilionekana kuwa tunakaribia kuwa watu 50 milioni.

Lakini pia hatuwezi kusahau mkasa wa ndege ya Ethiopia ulioua watu 157 mnamo mwezi Machi. Idadi kubwa ya abiria na wahudumu wa ndege hiyo walikuwa Wakenya. Mauti pia yalitupokonya watu maarufu, akiwemo aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Safaricom, Bw Bob Collymore.

Kisha kulikuwa na maporomoko ya ardhi yaliyoua zaidi ya watu 40 katika kaunti ya Pokot Magharibi, bila kusahau mkasa wa ajali katika kivuko cha Likoni.

Kwenye matukio haya, yapo ambalo tulikuwa na uwezo wa kuyazuia lakini hatukuchukua hatua zozote. Ajali za barabarani, maporomoko ya ardhi, watu kufa kwa njaa au mafuriko, ni mambo tunayoweza kuyazuia.

Mbali na idara za serikali, wananchi wana jukumu la kuhakikisha usalama wao.

Si hekima kwa mtu kujenga kwenye ukingo wa mto au chini ya mlima na maeneo tambarare. Hata serikali inapowaamuru watu waondoke, huanza kulalama na kuuliza waondoke waende wapi.

Mwaka tunaouanza kesho, yatupasa sote tuwajibike na kujiepusha na mambo yanayoweza kutuangamiza. Kila Mkenya akae chini na kutafakari kuhusu makosa aliyoyatenda mwaka 2019, kisha aweke azma ya kuwa hatayaruhusu yajirudie mwaka ujao.