Makala

TAHARIRI: Tunawapa wabunge alama ya 'E' kwa utendakazi

August 7th, 2018 1 min read

Na MHARIRI

AGOSTI 8, 2018 ni mwaka mmoja kamili tangu Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 mwaka 2017, ambapo mamilioni ya Wakenya walimiminika kwenye vituo vya uchaguzi kuwachagua viongozi wao.

Mwaka mmoja baadaye, mengi yamefanyika nchini, ambayo twapaswa kuyatathmnini kwa kina.

Mbali na Rais Uhuru Kenyatta kuwa na maridhiano na mpinzani wake mkuu Raila Odinga, hakujakuwa na uongozi mzuri kutoka kwa wanasiasa tuliochukua muda mwingi kwenye milolongo mirefu kuwapigia kura.

Masikitiko hasa ni kuhusu jinsi ambavyo wabunge 337 waliopigiwa kura na mwananchi hawajaonyesha uongozi unaostahili. Wengi wao wameamua kujihusisha katika siasa za mapema, huku wakijipiga vifua kuhusu nani anayeunga mkono Naibu wa rais William Ruto au anayesifu mwito wa kulipa deni la kisiasa.

Mwaka huu mmoja umegubikwa na matukio ya kuvunja moyo, yanayoonyesha wazi kuwa idadi kubwa ya wabunge hao si watu wanaoweka mbele maslahi ya mwananchi.

Kwa mfano kwenye suala zima la iwapo sukari iliyoingizwa nchini ina sumu au madini au la, limegawa wanasiasa hao.

Kuna madai kuwa ripoti ya awali iliyopendekezwa na wanachama wote wa kamati, baadaye iligeuzwa na kudhoofishwa kwa njia ambapo huenda isiwe na makali tena dhidi ya wanaoshukiwa kuhusika.

Hata mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayohusika na Biashara, Viwanda na Vyama vya Ushirika, Bw Kanini Kega, alishindwa kueleza ilikuwaje hata walioandika ripoti ya mwisho iliyowasilishwa bungeni wakabadili yaliyokubaliwa na wanakamati wote.

Lakini si hilo tu. Wabunge 20 walioamua kutumia pesa za mlipa ushuru kwenda kutazama mechi za Kombe la Dunia nchini Urusi, hadi sasa hawajaweza kuandika ripoti kuhusu walichojifunza au kufanya kwa manufaa ya mwananchi.

Bila kuona aibu, wabunge walijikusanya pamoja wiki mbili zilizopita kutaka kuwahoji wanahabari waliofichua jinsi ambavyo wengi wao wameamua kutumia nafasi zao kuhongwa ili kuwapendelea watu wanaohusishwa na ufisadi.

Hii ndiyo hali ambayo mwananchi anakumbana nayo tunapokamilisha mwaka mzina tangu tuwapeleke bungeni wanasiasa hao.

Kama ungekuwa mtihani, wabunge hao wangepata alama E.