Makala

TAHARIRI: Tusiache ligi yetu kuu ikaporomoka

November 23rd, 2019 2 min read

Na MHARIRI

KWA sasa mechi za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ziko katika hatari ya kukwama kutokana na ukosefu wa pesa.

Majuzi, baada ya klabu zipatazo saba kuomba kuwa ligi isimamishwe ili zitafute udhamini wa kuziwezesha kushiriki ligi hiyo bila masumbuko, kampuni ya Kenya Premier League ambayo husimamia ligi hiyo ilikataa ombi hilo.

Sababu hasa ya kukataa ombi hilo haikujulikana wazi lakini ni makisio yetu kuwa huenda KPL waliogopa kuchekwa na ulimwengu iwapo wangesimamisha ligi kwa kukosa pesa.

Hatua ya kukataa ombi hilo imechangia kuondolewa kwa klabu ya Sony Sugar katika ligi wiki hii. Pia kuna uwezekano wa klabu nyingine kadhaa zinazotatizika kifedha kuondolewa baadaye.

Haya yote yanapojiri, sote twafaa tujiulize, inakuwaje kuwa ligi ya Kenya haipati mdhamini ilhali klabu ndogondogo za Uingereza na kwingineko hasa barani Ulaya, hung’ang’aniwa sana kila panapozuka haja ya mdhamini?

Je, thamani ya ligi yetu ni ya kiwango cha chini kiasi hicho? Ama ni mienendo yetu ya kukosa uzalendo kama Wakenya inayotuponza?

Kutojitokeza kwa mdhamini, miezi mitatu baada ya mdhamini aliyekuwapo – SportPesa- kujiondoa, ni ishara kwamba thamani ya ligi yetu ni ndogo sana, kiasi kwamba sharti pafanyike jambo upesi iwezekanavyo ili kuikweza hadhi hiyo.

Unapoliangalia suala hili kwa msingi wa uzalendo, inakuwaje kuwa taifa hili ambalo ndilo injini ya kiuchumi ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, haliwezi kupata hata shirika moja la kibiashara lililo tayari kujitwika jukumu la kusimamia ligi kuu?

Kuna kampuni nyingi nchini zinazounda faida kubwa kubwa kama vile Safaricom, benki ya KCB, Benki ya Co-op, Equity na nyinginezo; je uzalendo wao uko wapi?

Mashirika haya yanafaa kufahamu kuwa faida hizo kubwa yanazopata yanatokana na jasho la Wakenya; hivyo basi pana haja ya kuziauni taasisi za umma zinapojipata kwenye mtanziko wa kifedha.

Sharti viongozi wa Shirikisho la Soka la Kenya wafikirie kwa kina jinsi ya kuinogesha ligi yetu ili matukio ya fedheha kama haya yasishuhudiwe tena.

Pia viongozi wa FKF wanafaa wajidadisi kwa swali; sababu gani hatuwezi kuwarejesha waliokuwa wadhamini wa zamani, SuperSport? Hamna linaloweza kufanyika ili warejeshwe katika udhamini?