TAHARIRI: Tusikubali hisia za kisiasa zivuruge amani

TAHARIRI: Tusikubali hisia za kisiasa zivuruge amani

NA MHARIRI

WAKENYA wameonyesha uvumilivu na utulivu mkubwa katika kipindi chote cha uchaguzi.

Baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza uamuzi kuhusu uchaguzi wa urais, tusiruhusu hisia zetu za kisiasa zianze kuvuruga utulivu huu ambao tumekuwa nao hadi sasa.

Ni kawaida kwa binadamu kupandwa na hisia wakati matarajio yake yasipotimika katika nyanja yoyote ile.

Hisia hizi ndizo zimekuwa zikitumiwa vibaya na wanasiasa katika chaguzi zilizopita, kuchochea jamii moja dhidi ya nyingine.

Matokeo yake ni fujo, ghasia, mauaji na uharibifu wa mali ambao tulikuwa tukiona katika kila kipindi cha chaguzi za miaka iliyopita.

Nchi hii ina sheria nzuri ambazo zimethibitika kutenda haki kwa walalamishi wanaohisi kudhulumiwa uchaguzini.

Kenya ilijizolea sifa mwaka wa 2017, wakati uamuzi wa kihistoria ulipotolewa kufutilia mbali uchaguzi wa urais ilipothibitika kwamba haukufikia viwango vya haki na uwazi ilivyotakikana.

Kwa hivyo, tusiwe wepesi wa kuanza kutumia mbinu zisizofaa kueleza hasira zetu iwapo imetokea kuwa tangazo la maamuzi kuhusu urais halikwenda jinsi tulivyotarajia.

Kila mwananchi aachie nafasi wagombeaji wenyewe na vyama vyao vya kisiasa kutumia mifumo iliyopo ya kisheria ikiwa wana malalamishi yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi.

Awali ilikuwa ishadhihirika kwamba mirengo miwili mikuu ya kisiasa, ambayo ni chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na Muungano wa Kenya Kwanza, ilikuwa tayari inaandaa mawakili wake kuelekea Mahakama ya Juu endapo kutakuwa na sababu za kutilia shaka matokeo ya uchaguzi wa urais.

Kwa msingi huu, wananchi wote wajue fujo na ghasia hazitasaidia kwa njia yoyote ile.

Athari zinazosababishwa na fujo huchukua miaka mingi kurekebishwa hasa kiuchumi.

Vilevile, maisha yanayopotezwa kila mara mashambulio yakitokea hayawezi kurudishwa.

Kila wakati siasa zinapoisha wananchi watabaki peke yao kujitafutia riziki.

Wenye biashara wataendelea kutegemea majirani ambao ndio wamekuwa wateja wao kwa miaka mingi, bila kujali mirengo ya kisiasa wala kabila.

Serikali itakayoingia mamlakani baada ya mshindi kutangazwa, pia ijitolee mhanga kuhakikisha kuwa, hakutakuwepo migawanyiko baina ya wananchi kuendelea mbele.

Viongozi walioshinda nyadhifa mbalimbali wajue kuwa mamlaka zao hazitakuwa na maana kama nchi haina utulivu.Kwa upande mwingine, wale walioshindwa wasiende kuchochea wananchi kuzua fujo bali wafuate sheria ikiwa wana malalamishi kuhusu matokeo.

  • Tags

You can share this post!

Man-City wasajili beki Sergio Gomez kujaza pengo la...

Siraj apigana kuhakikisha amevalia jezi ya Harambee Stars

T L