Makala

TAHARIRI: Tusilegeze kamba dhidi ya corona

April 28th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

HUKU Kenya ikionyesha dalili za kuanza kulegeza kanuni za kupambana na ueneaji virusi vya corona, inahitajika hamasisho ziendelee kutolewa kuhusu hatari ambayo ingali iko.

Kufikia sasa, hakuna dawa wala chanjo inayotambulika ambayo imepatikana kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 kimataifa.

Majaribio ya dawa na chanjo ambayo yamefanywa kufikia sasa hayajaleta mafanikio.

Vile vile, wataalamu wanasema hata dawa au chanjo ikipatikana sasa, itachukua muda mrefu mno kabla iidhinishwe kutumiwa kwa binadamu. Haya yanadhihirisha kuwa safari ingali ndefu katika vita vya kukabiliana na virusi hivyo. Hatua ya serikali kutoa kanuni zitakazosimamia ufunguzi wa mikahawa ni kwa minajili ya kuanza kurudisha biashara ili kupunguza madhara ya kiuchumi.

Kufikia sasa, biashara nyingi tayari zimepata hasara kubwa tangu mgonjwa wa kwanza wa coronavirus alipotangazwa kupatikana Kenya. Hali hii imefanya maelfu ya watu kote nchini wamepoteza kazi zao na hawana namna ya kupata riziki. Hatua zimepigwa kwa kutibu wagonjwa wapatao 114 kati ya 363 walioambukizwa, lakini hatuwezi kusahau vifo 14 ambavyo vilitokea. Kimataifa, nchi nyingi zimeanza kulegeza kanuni za kuepusha ueneaji wa virusi hivyo ili kuanza kuokoa uchumi.

Hatua chache tulizopiga kufika sasa hazifai kurudishwa nyuma kwa hivyo chochote kile kinachofanywa, kifanywe kwa tahadhari kubwa.

Wamiliki wa mikahawa itakayofunguliwa ni sharti wahakikishe kutakuwa na nidhamu kikamilifu miongoni mwa wahudumu na wateja wao. Hatungependa kuwa kama nchi ambazo zilidhani zimeanza kupata ushindi kisha maambukizi yakaanza tena kuongezeka.

Wito huu si kwa mikahawa pekee, kwani imebainika pia majengo kadhaa ya kibiashara ambayo yalikuwa yamefungwa, sasa yameanza kufunguliwa.

Ni jukumu la wahusika wote katika biashara hizi kutambua kwamba kile watakachofanya kitaokoa au kuhatarisha maisha yao wenyewe, wala sio ya wateja wao pekee.

Haitakuwa busara kwa mtu yeyote kusubiri kufuatiliwa na serikali ndipo atekeleze mipango ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona katika nchi hii.

Watu wasitazame hatua ya serikali kuanza kulegeza masharti kama idhinisho la umma kuanza kulegeza kamba katika vita hivi.