Makala

TAHARIRI: Tusilenge Waislamu katika vita dhidi ya ugaidi

January 23rd, 2019 1 min read

NA MHARIRI

Shambulio la wiki jana kwenye hoteli ya DusitD2 lilishtua si tu Kenya, bali ulimwengu mzima kwa namna magaidi walivyoivamia hoteli hiyo na kuua zaidi ya watu 20.

Ni tukio ambalo linapaswa kukashifiwa na kila Mkenya mpenda amani. Shambulio hilo lisitumiwe kupaka tope dini ya Kiislamu na Waislamu ambao tumeishi nao na miaka na mikaka. Tumetangamana nao kwa wema na hata kuoana na kuendeleza kizazi na wao.

Kudai kwamba Uislamu unaunga mkono ugaidi ni upotofu na kukosa kumakinikia matamshi yanayoweza kuvuruga umoja na udugu wetu kama Wakenya. Maafisa wa Usalama wanaosaka magaidi wasiwahangaishe waumini wa Kiislamu ambao hawana hatia, bali wawafichue magaidi hao na kuwaweka katika mizani ya haki, ili waathiriwa nao wapate haki yao.

Katika tukio la hivi majuzi na matukio mengine ya ugaidi kama vile lile la Westgate na Chuo Kikuu cha Garissa, ndugu zetu Waislamu waliungana na raia wengine nchini kuyakashifu matendo hayo ya kinyama yasiyo na utu.

Vyombo vya habari vilisaidia kusambaza ujumbe huu wa kizalendo. Ugaidi haujui dini wala kabila. Miongoni mwa waathiriwa wa ugaidi juzi walikuwa ndugu zetu Waislamu kwa majina Abdallah na Feisal nao walikuwa Waislamu, au sio?

Tumeona majina ya washukiwa wakuu katika shambulio la DusitD2 na mashambulio mengine yakiwa si majina ya Kiislamu pekee. Hivi ni kusema kwamba mtu yeyote aweza kupewa mafunzo ya itikadi kali akawa gaidi.

Kama ilivyoshadidia serikali na mashirika ya umma, sote tunapaswa kukaa ange na kuwafahamu majirani wetu ili kukitokea matukio kama haya, iwe rahisi kuwatambua. Tuheshimu dini zetu zote kwa manufaa ya kila mmoja.

Mola awape subira waliopoteza wapendwa wao katika uvamizi wa hivi punde, na waliojeruhiwa wapate nafuu ya haraka. Tuakatae kukatishwa na magaidi hawa hayawani na tushikamane tuwe ngao dhidi ya wale wanaotaka kutugawanya kwa misingi ya dini na kabila.