TAHARIRI: Tusiwe na pupa ya kurudisha kiboko

TAHARIRI: Tusiwe na pupa ya kurudisha kiboko

NA MHARIRI

PENDEKEZO la Wizara ya Elimu kwamba adhabu ya kuchapa wanafunzi kiboko irudishwe kisheria linaendelea kuibua hisia tofauti miongoni mwa umma.

Tatizo la utovu wa nidhamu kwa watoto katika kiwango cha kushtua si jambo geni katika nchi hii.Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na matukio ya kutisha yanayohusu uporaji, uharibifu wa mali, utumiaji wa mihadarati, ubakaji na hata mauaji ambapo wahusika ni watoto wa shule.

Sababu tofauti hutolewa na wadau mbalimbali kila mara matukio haya yanapoongezeka, kwa mfano hivi sasa ambapo tunayashuhudia kwa wingi katika pembe tofauti za nchi.

Shida inayotukumba kama taifa ni kuwa huwa tunaharakisha kubahatisha chanzo cha utovu wa nidhamu kufikia kiwango hicho cha kushtua.Utasikia kila aina ya mapendekezo kutoka kwa wadau tofauti, ndani na nje ya sekta ya elimu.

Hata hatua ya kuwasukuma watoto watundu jela kwa uhalifu wao inaonekana imeshindwa kufua dafu.Kwa sasa, huenda serikali ikaharakisha kurudisha adhabu ya kiboko kama inaamini hiyo ndiyo suluhu. Lakini jambo la busara ni kujiuliza kama kweli kiboko itasuluhisha hali tunayoshuhudia.

Kimsingi, wanaopendekeza adhabu ya kiboko wanaangalia jinsi maisha yalivyokuwa katika miaka ya themanini hadi tisini kabla adhabu hiyo ilipopigwa marufuku mwaka wa 2001.

Inafaa ieleweke kuwa katika miaka hiyo yote hadi sasa, hali imebadilika. Watoto wanavyokua sasa si kama ilivyokuwa katika miaka hiyo iliyopita.

Kuna mambo mengi ambayo watoto wanapitia katika enzi hii yanayofaa kuzingatiwa na wadau wote wanaotafuta suluhisho kuhusu utovu wa nidhamu.Mbinu za ulezi zinazotumiwa na wazazi enzi hii ni tofauti.

Vile vile, watoto hupokea habari nyingi mno kutoka kwa vyombo vya habari ikiwemo mtandani, ambazo pia huchangia tabia zao.

Masuala haya, pamoja na mengine mengi kuhusu mabadiliko ya mandhari ambayo watoto wanaishi ni lazima yazingatiwe wakati suluhisho inapotafutwa.

Msimamo wetu haumaanishi tunapinga adhabu ya kiboko, bali tunatoa tahadhari kwamba ni muhimu wadau wahakikishe hatua yoyote watakayochukua haitaharibu hali zaidi bali itarekebisha.

You can share this post!

Walimu waililia serikali iwalinde dhidi ya ugaidi

Corona imeathiri uwezo wa wanaume kuzalisha – Utafiti