TAHARIRI: Tutahadhari shule zisifungwe kaunti 13

TAHARIRI: Tutahadhari shule zisifungwe kaunti 13

KITENGO CHA UHARIRI

JANGA la Corona linapoendelea kuvuruga maisha ya watu katika pembe mbalimbali za dunia, nchini Kenya kuna changamoto mpya.

Kaunti 13 majuzi zilitajwa kama kitovu cha maradhi hayo tandavu.

Hofu imetanda katika maeneo haya kutokana na msambao wa aina mpya ya virusi vya corona vyenye asili ya India ambavyo vinahofiwa kuwa na makali kuliko aina ya awali.

Katika maeneo haya ambayo aghalabu ni Magharibi ya nchi pamoja na Nyanza, hospitali nyingi zimejaa na wahudumu wa afya wamelemewa na mzigo wa wagonjwa wengi kupindukia.

Ni katika mazingira haya ambako kuna shule nyingi zinazoendelea kujizatiti kukamilisha muhula wa tatu baada ya kalenda ya masomo kuvurugwa pakubwa mwaka uliopita. Hii ina maana kwamba ongezeko la corona katika kaunti hizi 13 linatishia kulemaza masomo kwa mara nyingine tena.

Wanafunzi wengi waliohojiwa wasema kwamba ombi lao kubwa ni kutotokea kwa tangazo jingine kwamba shule katika eneo husika zitafungwa tena. Baadhi yao walitishia kuacha kabisa masomo endapo hatua kama hii itachukuliwa. Wapo wanaosema endapo shule zitafungwa tena basi afadhali wajitose katika vibarua kusaka tonge.

Ni katika hali hii ya kuchanganyikiwa ambapo tunashauri kwamba hatua madhubuti zichukuliwe kuwakinga wanafunzi hawa ambao wamesalia tu na majuma machache kukamilisha muhula wao wa tatu ambao una umuhimu wa kuamua iwapo watasonga katika madarasa yafuatayo au la.

Wadau wote walimu na wazazi wakiwemo wanafaa kushiriki katika kunusuru hali hii. Kinachohitajika kufanyika si mambo makubwa. Ni mambo ya kimsingi tu. Kila mtu anashauriwa arejelee uzingatifu wa kanuni msingi kama vile kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa na kuhakikisha kwamba watu wanaepuka misongamano.

Walimu wanaofunza katika shule za mabweni wamakinike sana ili wasije wakawa wao ndio chanzo cha lawama. Kwamba uzembe wao katika kuwajibika uwatose maskini wanafunzi wasiotoka shuleni katika baa.

Wazazi wa wanafunzi katika shule za kutwa wahakikishe kwamba wanawahimiza wanao kuzingatia kanuni za kukabili corona mbali na wao wenyewe kuongoza kwa kuwa mfano mwema.

You can share this post!

Besigye achemkia Museveni kupanda kwa visa vya corona

Uhuru afinya raia usiku