Makala

TAHARIRI: Tutathmini maana halisi ya Valentino

February 14th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

ALHAMISI ya leo watu wengi duniani wanasherehekea siku ya wapendanao, maarufu kama Valentino. Sherehe hizi zinafanyika wakati mwafaka kutokana na haja ya kutathmini upya nini hasa maana ya mapenzi nyakati hizi tunazoishi.

Kumekuwepo na mabadiliko makubwa kote duniani ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, ambayo yanatoa ufafanuzi mpya kwa masuala mbalimbali yakiwemo mapenzi.

Kwa mfano siku hizi kumekuwepo na watu wa jinsi moja ambao wanadai kupendana, na jamii na mataifa mbalimbali zimewatambua hata kisheria. Kutokana na kutambulika huku watu wa jinsi moja, iwe mashoga ama wasagaji, wanafunga ndoa katika baadhi ya mataifa.

Baadhi ya wakazi wa Nairobi wakito damu eneo la Kencom Februari 14, 2019. Picha/ Peter Mburu

Lakini suala muhimu kwa siku ya Valentine ni mapenzi kati ya wanaume na wanawake. Hii ni kutokana na kuwa chimbuko la siku hii lilikuwa ni kuhusu mapenzi ya aina hii.

Tukumbuke kuwa mapenzi siku hizi yanakabiliwa na changamoto tele, jambo ambalo linazua maswali kuhusu hali ya familia na jamii yote kwa jumla, ikizingatiwa kuwa msingi wa taasisi hizi huanza katika mapenzi.

Siku hizi mapenzi kama yalivyoeleweka zamani kama uhusiano wa dhati kati ya mwanamume na mwanamke wakati wa shida na furaha, yamebadilika, na mapenzi ya siku hizi yanategemea zaidi fedha kuliko kujitolea kwa moyo – vijana wasio na pesa wanakosa wapenzi wa kuoa, ndoa zinavunjika pamoja na wapenzi kutoana uhai. Usherati pia unaonekana kukubalika katika jamii ya sasa.

Mwanamke akitoa damu Valentino Dei Kencom, Nairobi. Picha/ Peter Mburu

Matokeo ya ukosefu wa mapenzi ya dhati ni kuwepo kwa jamii yenye watu ambao hawajali wenzao, ambapo matunda yake ni ubinafsi, ufisadi, uhalifu, uongozi mbaya na maovu mengine ya kijamii.

Wale wanaotambua na kuenzi siku hii wanafaa wanapoelezea hisia zao kwa wanaodai kupenda kujiuliza mapenzi hayo yamejengwa kwenye msingi upi. Iwapo msingi wa mapenzi hayo ni pesa ama mali, basi wafahamu kuwa yamejengwa kwenye msingi hafifu na matokeo yake ni kilio siku za baadaye.

Pia mapenzi yaliyojengwa kwenye msingi wa uchu yanayumba na yatakuja kuporomoka siku moja.

Wakenya wasubiri zamu yao ya kutoa damu jijini Nairobi Valentino Dei. Picha/ Peter Mburu

Unapotuma maua na zawadi kwa wale unaodai kupenda, pia angazia iwapo kama kweli ndani ya moyo wako unamaanisha ujumbe ambao zawadi hizo zinapitisha.