Makala

TAHARIRI: Tuunge juhudi za kuukabili ufisadi

October 8th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

UFISADI ni janga ambalo limefanya Kenya kurudi nyuma kimaendeleo.

Pesa zinazostahili kutumika kwa manufaa ya umma, mara kwa mara zimekuwa zikiishia kwenye mifuko ya watu wachache walafi, wanaojitajirisha pamoja na washirika wao.

Kila kukicha, wafisadi huvumbua mbinu mpya za kukwepa kunaswa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), pamoja na wale wa polisi.

Kwa hiyo kuzinduliwa mwongozo mpya wa jinsi ya kukabiliana na watu hao, ni hatua inayofaa kuungwa mkono na wananchi. Ufisadi umekuwa kero lisilovumilika.

Kutokana na ufisadi, pesa zilizotengewa ununuzi wa gari la kubeba wagonjwa zinapotumiwa na watu wachache, watu hukosa magari ya umma ya kuwakimbiza hospitalini wanapokuwa na dharura ya kimatibabu.

Huko hospitalini, iwapo kutokana na ufisadi pesa za kununua dawa ziliibwa, hukosekana dawa nzuri za kutibia. Mwishowe, kama daktari alitumia hongo kupita mtihani wa udaktari, huishia kumpa mgonjwa dawa zisizostahili na pengine kusababisha kifo.

EACC chini ya Bw Twalib Mbarak na mwenyekiti Askofu Mkuu Mstaafu Eliud Wabukala, imeonyesha kujitolea sio tu kuwakabili wafisadi, bali pia kurejesha mali ya umma iliyoibwa.

Kwa mfano katika kipindi cha miaka mitano, imefanikiwa kurejesha mali ya ufisadi ya thamani ya Sh20 bilioni. Aidha ilitibua majaribio ya wizi wa mali ya umma ya thamani ya zaidi ya Sh100 bilioni.

Katika kipindi hicho hicho, EACC iliwapeleka kortini zaidi ya watu 1,000 ambapo 153 wamehukumiwa na kufungwa jela. Kesi nyingine 824 zinachunguzwa.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba kesi hizi ni zile zinazohusisha mamilioni ya pesa. Wananchi kwa upande wao, wanaweza kusaidia katika juhudi hizi kwa kukataa kutoa ‘kitu kidogo’ na kuwaripoti watu wengine wanaojihusisha na maovu haya.

Wakenya walidhihirisha kwamba wanaweza kutekeleza jukumu hili. Wakati serikali ilipofunga miji ya Nairobi na Mombasa, wakazi vijijini walikuwa wakiwaripoti watu waliofika mashinani. Kwa njia hiyo hiyo, wanaweza kupiga ripoti moja kwa moja kwa maafisa wa EACC kuhusu matukio yoyote ya ufisadi.

Miaka saba iliyopita, watu walichukua hatua dhidi ya wafisadi, wakiwemo maafisa wa polisi. Tunaweza kujitolea tena kuhakikisha kwamba tunakuwa ajenti wa maadili.