TAHARIRI: Tuwakatae wanasiasa wenye ndimi za chuki

TAHARIRI: Tuwakatae wanasiasa wenye ndimi za chuki

NA MHARIRI

MTINDO huu wa wanasiasa kujisahau wanapohutubia wafuasi wao kisha kuomba radhi baada ya kutoa matamshi ya uchochezi au kuyadunisha baadhi ya makundi katika jamii hauridhishi hata kidogo.

Matamshi anayotoa mwanasiasa anapopewa kipaza sauti ndio uhalisia wa msimamo wake kuhusu masuala anayozungumzia.

Kwa mfano, matamshi ya Seneta Cleophas Malala (Kakamega) kwamba kazi ya polisi ni kushika na kutumia bunduki pekee ni ya kusikitisha sana.

Bw Malala pia alinukuliwa akisema kuwa kinyume na taaluma nyingine, polisi hawana masomo ya kutosha.

Ijapokuwa Seneta huyo aliomba msamaha kutokana na matamshi hayo, hilo linaonyesha msimamo wake na dhana aliyo nayo kuwahusu polisi au makundi mengine katika jamii. Kila wakati uchaguzi unapokaribia, huwa tunawaona wanasiasa wakitoa kila aina ya matamshi na baadaye kuomba radhi kutokana na athari zake katika jamii.

Baadhi ya matamshi hayo ndiyo yamekuwa yakihusishwa na matatizo yaliyotukumba hapo awali nchini kama vile ghasia za baada ya uchaguzi tata wa 2007/2008.

Matamshi yayo hayo ndiyo yanahusishwa na ghasia zilizoshuhudiwa nchini mnamo 1992, 1997 na 2017.

Uchaguzi mkuu unapokaribia, wito mkuu kwa taasisi muhimu kama Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ni kutokubali baadhi ya ‘misamaha’ inayotolewa na wanasiasa, kwani matamshi yao yanaashiria misimamo yao halisi.

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Raila na Ruto kutumia ardhi kama chambo...

Walimu wataka vyumba vya kunyonyeshea vijengwe shuleni

T L