Makala

TAHARIRI: Uchunguzi wa mauaji uharakishwe

September 19th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

VISA vya utekaji nyara na mauaji, hasa ya watoto vimeongezeka katika siku za hivi karibuni na kila hatua zinapaswa kuchukuliwa na asasi zinazohusika na usalama kudhibiti hali hiyo.

Yamkini, kuna baadhi ya watu katika jamii yetu waliopoteza utu wao. Kisa cha hivi punde zaidi ni utekaji nyara na kisha mauaji ya mtoto Maribel Kapolon ambaye ni mwanawe hakimu mkuu mkazi wa mahakama za Githongo.

Ingawa ni mapema kubaini iwapo mauaji hayo ya kikatili yana uhusiano wowote na kazi ya mamake, ukweli ni kwamba, hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha uhayawani kama ule aliotendewa msichana huyo.

Ni macho ya nani yasiyolengalenga na machozi baada ya kutambua ukatili aliotendewa mtoto huyo? Ni moyo wa nani usiosononeka baada ya kutafakari kuhusu kilio cha mtoto huyo akijaribu kuwashawishi wauaji wake wanusuru nafsi yake?

Mauaji haya yanafuatia mengine ya kukeketa maini ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo, Sharon Otieno ambaye alichukuliwa mateka na kisha mwili wake ukapatikana umetelekezwa kichakani.

Ingawa visa hivi viwili ni vya uchungu kwa familia za waathiriwa na Wakenya kwa jumla, tunaamini maafisa wetu wa usalama wamepata mafunzo kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua kwa haraka.

Wataalamu wanahoji sababu za polisi kuchelea kuandama wahusika hasa baada ya simu kupigwa kudai fidia ya Sh500,000 kutoka kwa familia ya mtoto huyo.

Wengi wanaamini, kutokana na vifaa vya kisasa vya teknolojia ya mawasiliano, ni vigumu kwa wahalifu hao kukwepa mkono mrefu wa sheria. Hali ilikuwa hiyo hiyo katika mauaji ya Bi Otieno.

Baada ya mwandishi habari Barack Oduor kuponea kwa tundu la sindano na kuwapasha habari polisi kuhusu masaibu yake na Sharon, ukweli ni kwamba, utepetevu wa maafisa husika ulichangia mauti ya mwanafunzi huyo ambaye kifo chake kilishtua Wakenya.

Tunachosema hapa ni kwamba, wahalifu hawapaswi kuruhusiwa kusambaza hisia za woga na kuzua hofu katika jamii bila wasiwasi wa kuadhibiwa. Wale ambao hawathamini maisha ya binadamu wenzao hawapaswi kuwa na fursa ya kuendelea kutangamana na raia wengine wapenda amani.

Ukweli ni kwamba, yeyote anayechinja mtoto mdogo kama Matibel au kudunga kisu mjamzito kama Sharon amepoteza utu na hapaswi kamwe kuruhusiwa kufurahia uhuru na yote yanayoambatana na uraia wema.

Ni matumaini yetu kwamba, polisi watachukua hatua za haraka kuwanasa wahusika kwenye mauaji hayo yaliyotikisa nchi ili kuwasilisha ujumbe kwa wengine kuwa uhalifu haulipi!