TAHARIRI: Ufafanuzi zaidi kuhusu Gredi ya 7 wahitajika

TAHARIRI: Ufafanuzi zaidi kuhusu Gredi ya 7 wahitajika

NA MHARIRI

HATA ingawa serikali imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu jinsi wanafunzi wa Gredi ya 6 chini ya mfumo mpya wa elimu (CBC), watakavyovuka kutoka shule ya msingi hadi sekondari, ukweli ni kwamba bado kuna mianya kuhusu harakati hiyo inayofaa kuzibwa.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, mnamo Jumatano alisema kuwa wanafunzi hao wanaweza kujiunga na Gredi ya 7 (ambalo ni darasa la mwanzo la Sekondari ya Awali) katika shule za msingi au shule za sekondari za sasa.

Hata hivyo, pana mahitaji muhimu ambayo shule za sekondari za sasa zitalazimika kuyatimiza ili kutekeleza agizo hilo bila tatizo.

Kwa sasa shule za sekondari hazina madarasa ya watoto wa ziada, yaani hao wa Gredi ya 7, maadamu ilivyo kwa sasa darasa la chini la shule ya upili ni Kidato cha Kwanza.

Mwaka ujao, wanafunzi watakaokuwa wamefanya mtihani wa darasa la nane (KCPE) watatumia madarasa hayo na hivyo basi kuwaacha wale watakaojiunga na Sekondari ya Awali (Gredi ya 7) bila mahali pa kusomea isipokuwa iwapo shule hizo zitajitahidi mwaka huu kujenga madarasa ya ziada yatakayotumiwa na wanafunzi hao wa Gredi ya 7.

Lakini si madarasa tu, shule hizo pia zitahitaji walimu wa ziada kuwafunza watoto hao wa Gredi ya 7.

Kwa sasa shule nyingi zaidi ya asilimia 80 hazina walimu wa kutosha. Hii ina maana kuwa iwapo wanafunzi wa ziada watajiunga na shule hizo, walimu wengi watahitajika kuajiriwa ili kufaulisha utekelezaji wa majukumu ya ziada.

Hata hivyo, wanafunzi watakaoendeleza masomo yao katika shule za msingi za sasa, hawatakuwa na shida maadamu yapo madarasa ya kutosha kwa watoto wa Gredi ya 7 ambayo ndiyo Darasa la 7 kwa sasa.

Pia vitabu na nyenzo nyingine za ufundishaji zipo katika shule za msingi.

Kwa hivyo, itakuwa rahisi zaidi kwa wanafunzi hao kuendeleza masomo yao ya sekondari ya awali katika shule za msingi za sasa.

Hali inaweza kubadilika kwa shule za sekondari za sasa hapo baadaye ambapo taasisi hizo zinatarajiwa kubuni miundomsingi zaidi ya kuwasitiri wanafunzi wa Gredi ya 7, 8 na 9 (gredi tatu zinazoitwa Sekondari ya Awali).

Tatizo la pili katika ufafanuzi wa Prof Magoha ni kusisitiza kuwa wanafunzi hao wasiwe wa masomo ya malazi. Yaani wawe wakisoma kwa mfumo wa kutwa pekee.

Tunahisi kuwa hilo la kutwa na malazi lingeachiwa shule na wazazi wenyewe waamue.

Ikumbukwe kuwa hata kwa sasa kunazo shule nyingi zaidi nchini ambazo zinawapa wanafunzi wa shule za msingi utaratibu wa masomo ya malazi.

You can share this post!

KIKOLEZO: Riri, huyo Kanairo

‘Muuaji’ De Bruyne aweka Man City pazuri

T L