Makala

TAHARIRI: Ukatili wa polisi lazima ukome

June 9th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

UFICHUZI kuwa kuna kesi zaidi ya 120 mahakamani kuhusu ukatili wa polisi dhidi ya raia unaleta matumaini kwa waathiriwa kwamba huenda wakatendewa haki.

Hata hivyo, kwa kuzingatia matukio ya miaka iliyopita, kuna uwezekano haki isitendeke kwa waathiriwa hao. Hii ni kwa sababu kesi chache aina hii ambazo zimefanikiwa kukamilika haraka hadi maafisa husika wakaadhibiwa kisheria.

Msimamo wa Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i kwamba polisi yeyote anayetuhumiwa kuhusika katika ukatili dhidi ya raia atabeba msalaba wake mwenyewe, unafaa kuthibitishwa kwa vitendo.

Wakati mwingi malalamishi yanapotolewa kuhusu jinsi polisi wanavyotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia, hutakosa kusikia wakubwa wao wakiwatetea.

Ni utetezi huu ambao hufanya wengi kufa moyo hata wa kufuatilia kesi zinazohusu ukatili, kwani machoni mwao wanaona hawana uwezo ikilinganishwa na polisi watakaotetewa na serikali.

Ukiukaji wa haki za binadamu kwa idara ya polisi umeonekana kuongezeka sana katika kipindi chote ambapo taifa linapambana dhidi ya janga la corona sawa na ulimwengu mzima unavyofanya.

Hii ni aibu kwa taifa kwani ni jambo ambalo limevutia hamaki hadi kwa mashirika ya kimataifa yanayotetea haki za binadamu.

Wito wa kutaka idara ya polisi ikomeshe vitendo vya kupiga, kujeruhi na hata kuua raia wasio na hatia hutolewa mara kwa mara kila mwaka lakini hakuna hatua zinazochukuliwa na wakuu husika.

Tumeshuhudia sheria za polisi zikirekebishwa na pia kanuni zikifanyiwa marekebisho ili kubadilisha mienendo ya maafisa.

Wakati Inspekta Jenerali Hilary Mutyambai alipochukua uongozi wa kikosi cha polisi, ilitarajiwa pengine mambo yangebadilika akishirikiana na Dkt Matiang’i.

Inasikitisha kuwa, kufikia sasa, mambo ni yale yale ya raia kuumia mikononi mwa kikosi kinachostahili kuwalinda.

Kunao watetezi wa polisi ambao husisitiza kuwa matukio ya ukatili ni machache ikilinganishwa na mema ambayo maafisa hao hufanya.

Hakuna utetezi wa kiwango chochote ambao unaweza kukubaliwa wakati tunapozungumzia mauaji ya watu wasio na hatia. Ni sharti tukomeshe ukatili huo sasa.