TAHARIRI: Tuonyeshe ukomavu wa demokrasia

TAHARIRI: Tuonyeshe ukomavu wa demokrasia

KITENGO CHA UHARIRI

UKOMAVU wa kisiasa ambao wakazi wa Eldoret walionyesha wakati kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alitembelea mji huo kuuza sera zake unafaa kuigwa na wanasiasa na wakazi wa maeneo mengine.

Wakazi hao walidumisha amani na kumsikiliza Bw Odinga licha ya kuwa ni kaunti ya nyumbani ya mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi wa urais mwaka ujao Naibu Rais William Ruto.

Viongozi wa eneo hilo walikuwa wamehimiza wakazi kumkaribisha Bw Odinga na msafara wake.

Huu ndio ukomavu wa demokrasia ambao viongozi wetu wa kisiasa wanafaa kuonyesha wakati wa kampeni za uchaguzi, kwenye uchaguzi na baada ya matokeo kutangazwa ili kuhakikisha nchi haivurugiki.

Kwa kawaida, ghasia za kisiasa huwa zimepangwa na kuchochewa na viongozi na wasipofanya hivyo, hakuwezi kuwa na hofu.

Wawekezaji wengi huwa wanahama Kenya au kufunga biashara zao kila uchaguzi mkuu unapokaribia lakini mambo yanaweza kuwa tofauti hali iliyoonekana Eldoret ikidumishwa kote nchini.

Imesemwa mara nyingi kwamba msimu wa uchaguzi na viongozi huja na kwenda na huwa nchi inabakia. Hii inafaa kuwa kauli mbiu ya kila Mkenya wakati huu wa siasa za uchaguzi mkuu.

Viongozi wote wa kisiasa na washirika wao wanafaa kutambua kuwa nchi ni kubwa kuliko tamaa yao ya uongozi. Wanafaa kuelewa kwamba watahitaji wakazi wa maeneo yao hata baada ya uchaguzi na mtu mmoja anapofariki kwenye ghasia za uchaguzi, huwa ni kura zao zinazopungua na nchi kupata hasara.

Ili kudumisha yaliyoshuhudiwa Eldoret, viongozi wa kisiasa wanafaa kuhubiri amani kwa dhati. Hii ni kwa sababu imeripotiwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakihubiri amani mchana na kuchochea jamii zao usiku.

Vijana nao wanafaa kukataa kutumiwa na wanasiasa. Wawapuuze na kuwakataa wale wanaowalipa kuzua ghasia katika mikutano ya kisiasa ya wapinzani wao.

Wasikilize sera za kila mmoja na kufanya uamuzi wao wenyewe.

Kufanya hivi na kufuata mkondo wa sheria wanasiasa wasiporidhika na matokeo, Kenya itakuwa imeingia katika ligi ya mataifa yaliyo na demokrasia zilizokomaa. Hii itachochea ukuaji wa uchumi kwa kuwa shughuli hazitavurugwa na wawekezaji watakuwa na imani na nchi yetu.

You can share this post!

Weta aamua ni Lusaka tosha ugavana 2022

Uthabiti wa Chelsea ni mtihani mgumu kwa wapinzani wao...

T L