Makala

TAHARIRI: Ulegevu umerudi barabarani

December 12th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

Hata ingawa Wakenya wengi walichangamkia hatua ya serikali kuanza kutekeleza upya kanuni za barabarani almaarufu Sheria za Michuki hivi majuzi, harakati hiyo imeanza kuchukua mkondo wa kusikitisha na kuhofisha.

Utekelezaji huo uliotangazwa na kutekelezwa na Wizara za Uchukuzi na Usalama wa Ndani, sasa umegeuka kuwa njia haramu ya kiuchumi wanayotumia maafisa wa polisi kufyonza mwananchi pesa.

Hii ndiyo maana licha ya msisitizo wa kutekelezwa kwa sheria hizo, ajali za kiholela zimeanza kurejea katika barabara zetu. Katika muda wa siku mbili hadi kufikia jana, zaidi ya wasafiri 10 walikuwa wameaga dunia kwenye ajali za barabarani.

Japo sheria hizo zilizolenga kupunguza vifo na majeraha hasa katika msimu huu wa Krismasi, matukio hayo ya jana yanadhihirisha kuwa bado kuna kasoro.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa polisi wa trafiki wamezembea katika kuzitekeleza au wengi wao wamezamia rushwa na kuruhusu madereva wasiojali pamoja na magari mabovu kuendelea kuhudumu barabarani.

Itakuwa bora Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i na mwenzake wa Uchukuzi Bw James Macharia kukaza kamba kuhusu utekelezaji wa sheria hizi ili kuokoa maisha zaidi ambayo huenda yakaangamia katika msimu huu wa sikukuu.

Sharti visa vya polisi wa trafiki kuendelea kula hongo barabarani viishe lau sivyo, mwananchi wa kawaida ataendelea kuumia kwa kutozwa hongo na kuhasirika panapotokea ajali hizi zinazoweza kuzuilika.

Ni muhimu madereva watundu hasa wale wa malori ya kusafirisha mizigo mizito wakamatwe na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Wengi wao wameripotiwa kuendesha magari yao kiholela na hivyo kusababisha ajali nyingi za barabarani.

Pia madereva wa magari ya uchukuzi wa abiria lazima wafuate sheria kikamilifu. Wengi wao wamesemekana kuendesha magari yao wakiwa walevi bila kuzingatia sheria za trafiki. Baadhi hawapumziki wanapong’ang’ania kupeleka wasafiri mashambani wanaokwenda kwa sherehe hizi za Krismani na Mwaka Mpya.

Magari mabovu yasiyostahili kuwepo barabarani vilevile yanahudumu na hivyo kuweka maisha ya abiria hatarini. Sharti magari yote yanayohudumu hasa katika msimu huu wa pilkapilka tele yawe yanayostahili kutumika barabarani.