TAHARIRI: Umakinifu wahitajika sherehe zikinukia

TAHARIRI: Umakinifu wahitajika sherehe zikinukia

KITENGO cha UHARIRI

Tunaingia wiki ya Krismasi na ni wakati wa kuhimiza uangalifu katika nyanja mbali mbali za kimaisha na kijamii.Kwanza, ikiwa ndio muda wa kusafiri kwa wengi, nyakati kama hizi hushuhudia visa vingi vya wizi na uvunjaji nyumba miongoni mwa visa vingine vya utovu wa usalama.

Wahuni wanajua watu wengi wamesafiri kwenda likizoni mashambani au kwingineko hivyo nyumba nyingi za makazi na za kibiashara hujikuta kulengwa na wahalifu. Ni vyema kuhakikisha kwamba kabla ya kutia kufuli langoni na kuondoka, uwe umeweka mikakati mingineyo ya kiusalama kama vile kuajiri bawabu au mlinzi wa kulinda vitu vyako vya thamani.

Kwa bahati mbaya, huu pia huwa wakati ambapo ajali nyingi za barabarani hutokea. Mara kwa mara ajali hizo zimehusishwa na pupa ya madereva wanaotaka kufika maeneo wanakoenda upesi ili waweze kufanya safari nyingi kuliko kawaida kutokana na wingi wa abiria. Nyakati zingine ni wenye magari wanaoongozwa na ulafi kiasi kwamba wanakataa kuwapa madereva muda mzuri wa kupumzika kabla ya kuanza safari.

Aidha, muda mwingine ni polisi wa trafiki wanaolaumiwa kwa kukosa kufanya kazi yao barabarani kwa kukubali hongo ili kuachilia gari bovu au linaloendeshwa kwa kasi kupita kiasi kuendelea na safari hivyo kuhatarisha maisha ya wengi. Inasikitisha mno kuona ajali hizi zikizusisha hata wanafunzi wanaotoka shule, kama ilivyoshuhudiwa katika eneo la Kambiti, Murang’a, Jumamosi ambapo maisha ya wanafunzi watatu yalikatizwa ghafla barabarani asubuhi.

Hakika, hakuna jambo lolote la dharura duniani, linaloweza kuwa muhimu kuliko maisha ya binadamu kwa hivyo yeyote aliye kwenye kiti cha dereva msimu huu wa Krismasi anastahili akumbuke kwamba amebeba roho za watoto, kina mama, wazee wanaotegemewa na familia zao na kwamba ni wajibu wake kuhakikisha amefanya kila awezalo kuwafikisha salama wanakoenda.

Uangalifu mwingine bila shaka ni kwa wazazi ambao wamepambana na mwaka mgumu katika kalenda ya shule, mwaka ambao ulishuhudia mihula minne iliyowakamua rasilmali nyingi za kifedha.Na sasa, punde baada ya Mwaka Mpya, muhula mwingine mpya nao unaanza na kama kawaida jukumu la kutafuta karo, sare za shule na mahitaji mengine linawasubiri.

Hivyo basi, hata wanaposherehekea kufunga mwaka, wazazi wahakikishe wamebakiza fedha za kuendeleza maslahi ya watoto wao kielimu

You can share this post!

Ruto, Raila wararuana Mombasa

Jumwa asukumwa awe naibu kiongozi UDA

T L