Makala

TAHARIRI: Umma usitwikwe mzigo wa madeni

February 20th, 2018 2 min read

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Patrick Njoroge. Deni la Kenya kwa sasa linakaribia Sh4 trilioni, hilo likimaanisha kwamba kiwastani, kila Mkenya ana wastani wa deni la Sh100,000 Picha/ Maktaba

Na MHARIRI

SERIKALI inapaswa kuzingatia ushauri wa mashirika ya kifedha kubuni mikakati ambayo itaipunguzia nchi deni la kitaifa.

Ushauri huo umetolewa na shirika la kifedha la Cytonn, ambalo limeonya kwamba Wakenya wanapaswa kuwa na hofu kutokana na kiwango kikubwa cha deni hilo, ambalo linaendelea kuongezeka kila kuchao.

Kulingana na ripoti kadhaa ambazo zimetolewa na mashirika mbalimbali ya kifedha, deni la Kenya kwa sasa linakaribia Sh4 trilioni, hilo likimaanisha kwamba kiwastani, kila Mkenya ana wastani wa deni la Sh100,000.

Kimsingi, huu ni mwelekeo wa kutia hofu, ikizingatiwa kwamba Kenya ingali taifa changa ambalo uchumi wake ni wa kiwango cha wastani.

Uchumi wetu ni mdogo sana, ikilinganishwa na nchi kama Amerika, Uingereza, Uchina, Japan, Ujerumani kati ya zingine.
Utathmini wa kina wa sababu kuu za ustawi wa chumi hizo unabainisha kwamba mojawapo ya nguzo kuu huwa ni kudhibiti deni la kitaifa la nchi.

Aidha, hilo huziwezesha sana nchi hizo kuendeleza mipango yake ya kimaendeleo bila changamoto za kifedha kwani huwa hazina matatizo kupata usaidizi kutoka kwa mashirika kama Benki Kuu ya Dunia ama Shirika la Kimataifa la Kifedha (IMF).

Hata hivyo, makosa mengi ya nchi zinazostawi ni kuwa, huwa zinachukua mikopo mikubwa kuwekeza katika miundomsingi, ila fedha nyingi hupotelea katika sakata za ufisadi.

 

Kisiki

Na ikiwa dhahiri kwamba Kenya imekuwa ikichukua mikopo mingi kuwekeza katika miundomsingi ya kuistawisha kiuchumi, pana haja kubwa kwa serikali kutathmini njia za kuhakikisha kuwa deni hilo haligeuki kuwa kisiki wa wananchi.

Njia ya kwanza ya kuhakikisha hayo ni kuwianisha Ajenda Nne za Maendeleo za Serikali na mikakati ambayo itachangia pakubwa katika uzalishaji wa fedha, ambazo zitaisaidia nchi kulipa madeni hayo kwa mapato yake yenyewe.

Pia, lazima ihakikishe kwamba wanaopatikana wakishiriki katika ufisadi wanakabiliwa vikali ili kuhimiza hali ya uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.

Hayo ndiyo yatahakikisha kwamba hatujipati katika mgogoro wa kifedha, kama ilivyojipata Ugiriki kwa kukosa kudhibiti deni lake la kitaifa.