Makala

TAHARIRI: Umwagaji damu barabarani ukome

October 11th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

HUKU nchi ikiendelea kuombeleza umwagikaji damu kupitia ajali mbaya zaidi ya hivi punde kuwahi kutokea; katika barabara kuu ya Kisumu – Muhoroni ambapo abiria 55 walipoteza maisha yao, swali kuu linaloibuka ni je, janga hili sugu litadhibitiwa lini?

Ripoti za kuvunja moyo ni kuwa ni wachache tu ambao waliweza kunusurika katika maafa hayo ikilinganishwa na walioangamia.

Huku idara ya polisi kwa ushirikiano na vitengo vingine husika vikiendelea kupekua na kukagua ili kutambua kilichosababisha ajali hiyo, hoja tatu muhimu zimejitokeza kutokana na abiria walionusurika.

Kulingana na mkuu wa Halmashauri ya Kitaifa ya Usalama ya Uchukuzi – NTSA, Bw Francis Meja, gari hilo la Western Cross Express halikuwa na leseni ya kubeba abiria usiku.

Pili, mmoja wa walionusurika alisema kwamba gari hilo lilikuwa lmebeba abiria 70 wa ziada huku makondakta wakiwanyamazisha wakati abiria hao walipolalamikia hali hiyo. Haikutosha hilo bali waliwatolea vitisho walionung’unika.

Tatu, Naibu Rais William Ruto katika risala za rambirambi kwa waliofariki ajalini humo, alisisitiza kwamba madereva wanafaa kuzingatia sheria za barabarani ili kujiepusha na mauti haya ya kuhofisha.

Bila shaka alimaanisha kuwa madereva hao waliendelea kukiuka kanuni hizo bila kujali kamwe.

Takwimu kutoka kwa idara hiyo, zinaonyesha kwamba kutoka Januari mwaka huu kufikia sasa, jumla ya watu 2,345 wameangamia ikiwa bado mwaka wenyewe haujakamilika.

Ajabu ni kwamba, ikilinganishwa na mwaka uliopita, idadi ya waliofariki imeongezeka kwa asilimia nane.

Serikali na idara husika hazitaweza kujiondolea lawama kwa mujibu wa ripoti zilizofichuka. Ikiwa gari hilo halikuwa na idhini ya kubeba abiria usiku, basi ilikuwaje likafanya hivyo bila kujulikana?

Inamaanisha kwamba suala hili lingekuwa limetatuliwa zamani, la sivyo kuna baadhi ya maafisa ambao hawatekelezi majukumu yao.

Vivyo hivyo habari kuhusu kubeba abiria kupita kiasi ni za kushangaza kwani kuna vizuizi vingi vya maafisa wa polisi ambavyo vimewekwa karibu kila barabara nchini na haijulikana ni kwa jinsi gani gari hili lilikwepa mtego wa maafisa hawa. Jinsi basi hilo lilivyoweza kupenya ni kitendawili kisichoweza kuteguliwa kufikia sasa.

Kwa ufupi, serikali inafaa kuzinduka usingizini na kuanza kusaka wavunjaji sheria za barabarani bila kusaza yeyote.

Hata hivyo, ni wajibu wa kila Mkenya kukabili janga hili kwa njia yoyote ile iwe ni kutoa ripoti kuhusu madereva waasi au kuepuka magari yaliyojaa abiria.