Makala

TAHARIRI: Unajisi shuleni ukabiliwe vikali

June 5th, 2018 2 min read

Na MHARIRI

KISA cha mwanafunzi kunajisiwa katika shule ya wasichana ya Moi jijini Nairobi ni dalili tu ya jinsi wanafunzi wanaendelea kufanyiwa unyama na watu ambao wameaminiwa na wazazi kulinda watoto wao.

Pia, polisi wa eneo la Kieni Mashariki, Kaunti ya Nyeri wanamtafuta mwalimu aliyedaiwa kumnajisi msichana wa darasa la nane.

Uchunguzi wa matibabu ulithibitisha kwamba msichana huyo wa shule iliyo Naromoru alinajisiwa.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, maafisa wa elimu wanachunguza mwalimu mkuu wa shule moja ya eneo la Taveta baada ya madai kuzuka kuwa alikuwa akilawiti wanafunzi katika eneo lake la kazi la awali. Ukweli mchungu ni kuwa visa vingi kama hivyo vinashuhudiwa katika shule nyingi mashinani bila kuripotiwa kwa maafisa wa usalama au hata kwa wazazi.

Siku chache zilizopita, walimu wawili wa shule moja ya msingi katika kaunti ya Nyandarua, walishirikiana na mwenzao wa tatu kumjeruhi mtoto mdogo katika sehemu zake nyeti.

Madaktari katika hospitali ya rufaa ya Nyahururu walithibitisha kuwa mtoto huyo aliraruliwa sentimita sita katika korodani. Unyama huu ni kimoja kati ya visa vingi vya unyama vinavyoendelezwa na walimu katika shule za umma nchini.

Ni jambo la kuudhi kwamba watu waliopewa jukumu la kuwaelimisha na kuwalinda watoto katika shule zetu za umma wanageuka na kuwa makatili.

Lililo wazi ni kuwa visa hivi vinatokea katika shule za umma ambapo kuna idadi kubwa ya wanafunzi.

Wakati umefika kwa Wizara ya Elimu kupitia Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuchukua hatua za haraka na kuchunguza walimu pamoja na watu wanaotaka kuwa walimu.

Itakuwa muhimu kwa kila afisa wa TSC anayesimamia kaunti kuwasilisha ripoti kuhusu tabia za walimu baada ya kipindi fulani kwa mwaka.

Ulawiti na unajisi wa wanafunzi shuleni sio tu ukiukaji wa maadili ya utendakazi wa walimu, lakini pia ni uvunjaji wa sheria kuhusu haki za watoto. TSC inapaswa kuwachukulia hatua kali walimu wote waliohusika katika visa vyote vya kuwadhulumu wanafunzi.

Itakuwa vyema kwa polisi na idara ya mahakama kuharakisha kuadhibiwa kwa washukiwa.

Ni Gazeti la Kampuni ya Nation Media Group
Mkurugenzi Mkuu: STEPHEN GITAGAMA
Mhariri Mkuu: TOM MSHINDI
Mhariri : PETER NGARE